Assalaam Alaykum,

 

Ufuatao ni utenzi unaoeleza kisa cha mtume wa Mwenyezi Mungu, Sayyidna Yusuf ALAYHI SALAAM. Utenzi huu umetungwa na Sh. Said Karama kutoka Lamu.

 

UTENZI WA KISA CHA NABII YUSUF (A.S.)

 

            Mtungaji : Said Karama  -  Lamu

 

 

    1.    Bisimilahi Kahari, Ya Rabi Mola Jabari, Mmoja uso akhiri, Wala mwanzo kuanzia

 

    2.    Naanza kwa lako jina, Mola wetu Subuhana, Mtukufu wetu Bwana, Wa pili asotokea

 

    3.    Twamsalia kaumu, Sote ndugu Isilamu, Mtume Bani Hashimu, Sayyidil Arabia

 

    4.    Sote Rabi Ya Rahimu, Twamsalia Hashimu, Na tunu nyingi salamu, Twamtakia nabiya

 

    5.    Nina kisa maarufu, Cha tumwa wake Latifu, Mtume mwema Yusufu, Wao Isirailia

 

    6.    Mtume wake Wahabu, Yusufu tumwa Habibu, Baba yake Yaakubu, Jinale tawatajia

 

    7.    Mzazi wake wa pili, Jinale ni kama hili, Aitwa bibi Rahili, Mtukufu wa muruwa

 

    8.    Yusufu ndie Rasuli, Aloletwa na Jalali, Kwa bani Isiraili, Kaumu isosikia

 

    9.    Nduguze kuwahisabu, Kwa majina ni taabu, Samahani masahibu, Idadi tawatajia

 

    10.    Ana kumi wa awali, Kwa baba na mama mbali, Na mdogo ni Rakili, Kwa baba na mama pia

 

    11.    Walikuwa majabari, Wasiogopa shari, Shujaa walo hodari, Dhiki ikiwafikia

 

    12.    Alipokwisha kuzawa, Na ndugu wakachukiwa, Wamuhasidi na ngowa, Maradhi yalokomaa

 

    13.    Sababu yeye kwa kweli, Alikua na jamali, Uzuri wake rasuli, Akipendeza nabiya

 

    14.    Ni mrembo mtulivu, Mwenye busara mwerevu, Na mwilini hana kovu, Uzuri umezidia

 

    15.    Yusufu alipokaza, Kwa wazazi kupendeza, Ndugu yakawachukiza, Mabaya kukusudia

 

    16.    Ndugu walifanya wivu, Na kila la uwerevu, Wamtendee uovu, Kumwangamiza dunia

 

    17.    Siku moja ya utoto, Amelala hako mato, Yusufu kaota ndoto, Ajabu nawaambia

 

    18.    Ndoto hiyo ya kioja, Jua na mwezi pamoja, Na nyota kumi na moja, Vyote kumsujudia

 

    19.    Muda alipogutuka, Hapo alipoamka, Alikimbia haraka, Kwa baba kumwelezea

 

    20.    baba kwa wake ujuzi, Akaifahamu wazi, Ndoto ya jua na mwezi, Na nyota kumi na moya

 

    21.    Na baba asinyamaze, Ndipo amsisitize, Mwanangu siwaeleze, Nduguzo nakuusia

 

    22.    Mwanangu stahamili, Siwaambie asili, Yusufu usikubali, Siri ya ndoto zuwia

 

    23.    Mungu atakukhitari, Akufunze tahariri, Ya ndoto na ya khabari, Waja wasizozijua

 

    24.    Hapo ndipo auladi, Hao kumi mahasidi, Ikashtadi hasadi, Wakawa na jicho baya

 

    25.    Hasadi ya jicho ovu, Kwa kumuonea wivu, Ili wamtenze nguvu, Yusufu mwema nabiya

 

    26.    Ndio waliokutana, Wote ashara vijana, Wasijizuie tena, Moyoni kuvumilia

 

    27.    Faragha walionana, Wote kushauriana, Mwisho wakasikizana, Maovu kuazimia

 

    28.    Wakatoka taratibu, Vijana hao kidhabu, Wakenda kwa Yaakubu, Baba yao kumwambia

 

    29.    Wakafika pasi khofu, Maneno kumuarifu, Kwa kumtaka Yusufu, Ruhusa kumuombea

 

    30.    Wamtaka ndugu yao, Yusufu mdogo wao, Ili asafiri nao, Huko wanakokwendea

 

    31.    Hila waliyoisema, Kwa wao mtu mzima, Ni Yusufu kuandama, Kwenda kucheza pamoya

 

    32.    Hapo baba kashangaa, Na kwanza akakataa, Akajua ni hadaa, Wana walomwelezea

 

    33.    Maana alitambua, Hila yao kuijua, Yusufu wamchukua, Lakini hatarejea

 

    34.    Mola aliyoandika, Ni uongo kufutika, Ni lazima kutendeka, Kwani yote yamwelea

 

    35.    Na baba kwa takilifu, Ya wanawe wapotofu, Moyo ukafanya khofu, Lakini kavumilia

 

    36.    Ikawa hapana budi, Baba yao kuburudi, Akamtoa fuadi, Yusufu kuwaachia 

 

    37.    Vijana wakaondoka, Na mji wakautoka, Pamoja na muhibbuka, Yusufu tumwa Jalia

 

    38.    Wakawa wasafarini, Wapotelea porini, Na huku wamachungani, Walisha katika njia

 

    39.    Wakawasili makini, Kando ya mji njiani, Kwenye mji Dausani, Mji walioingia

 

    40.    Kufikia kisimani, Mmoja wa ikhiwani, Ambae ni wa mwanzoni, Umri alozidia

 

    41.    Akalitoa shauri, Kuwapa ndugu khabari, Akasema jambo zuri, Yusufu kumtendea

 

    42.    Mimi katu sikubali, Tulivyowaza awali, Ni lazima liwe hili, Jengine sitoridhia

 

    43.    Yusufu tusimuweni, Sote na tumshikeni, Tumtupe kisimani, Haya kwake ni kifaya

 

    44.    Ikawa budi hawana, Asili kutoshindana, Mkubwa aloyasema, Wadogo wakatikiya

 

    45.    Hapo tena kwa upesi, Wakamvua libasi, Ambayo ndio khalisi, Yusufu alovalia

 

    46.    Na kisha wakamshika, Wakamtupa haraka, Kwenye kisima cha nyoka, Kirefu chenye udhia

 

    47.    Kwa uwezo wa Rabuka, Hata si robo dakika, Jibrili akashuka, Ajabu ilotokea

 

    48.    Kufumba na kufumbua, Jibrili keshatua, Yusufu kumuokoa, Kabla hajaumia

 

    49.    Jibrili kamnyaka, Kabla chini kufika, Taratibu kamuweka, Mahali pema nabiya

 

    50.    Baada ya kutendeka, Kisa hiki kufanyika, Nduguze wakatoroka, Wakaanza kukimbia

 

    51.    Wenda wakifurahika, Waongea wakicheka, Wakajua kwa hakika, Yusufu keshajifia

 

    52.    Kumbe wamehadaika, Na bure kuadhirika, Na Yusufu hana shaka, Bukheri kajikalia

 

    53.    Hata kwa muda saghiri, Wakazuka wasafiri, Wenda mji wa Misiri, Wa katika yao njia

 

    54.    Ulikua msafara, Ulotimia imara, Wafanyaji biashara, Wasafiri wa ngamia

 

    55.    Hapo bila ya kungoja, Maji ndio yao haja, Wakamtuma mmoja, Maji kwenda watekea

 

    56.    Ndoo ikashika papo, Yusufu hapo alipo, Akashika papo hapo, Kamba ilomlekea

 

    57.    Kamba alipoipata, Akawa yuwaivuta, Na aliyeikamata, Uoga ukamwingia

 

    58.    Uoga na taharuki, Kwa kamba yake kusaki, Ndoo haitaharuki, Yusufu ameigwia

 

    59.    Katizama kutafiti, Kujua kilo tiati, Mara ikaja sauti, Kisimani kutokea

 

    60.    Kwa nguvu zake Kahari, Ndipo tena wasafiri, Hapo pasi kusubiri, Kutafuta kila ndia 

 

    61.    Ikawa ni pata shika, Waume kushughulika, Kamba zimekusanyika, Kisimani zangojea

 

    62.    Yusufu kwenye kisima, Akatolewa mzima, Ameokoka salama, Kama hakutumbukia

 

    63.    Basi hapo mtukufu, Mtume mwema Yusufu, Akawa yukwenye safu, Na wasafiri pamoya

 

    64.    Wakawa wasafarini, Na Yusufu yukundini, Hadi Misiri mjini, Wendako kuwasilia

 

    65.    Nduguze bila kungoja, Wote kumi kwa umoja, Kutimia yao haja, Walianza kurejea

 

    66.    Wenda bila wasiwasi, Ndiani wakihadisi, Pamoja nayo qamisi, Walomvua nabiya

 

    67.    Na mipango walofanya, Ya hila na kudanganya, Ili kwamba kuwaponya, Baba wanapomwambia

 

    68.    Walingia kwenye kazi, Ya kumkamata mbuzi, Kumchinja kwa ukuzi, Ovu lao kufidia

 

    69.    Wakaipaka libasi, Yusufu yake qamisi, Kwa hiyo damu najisi, Ya mbuzi walomuua

 

    70.    Nyumbani wakawasili, Na baba kumkabili, Na la kwanza ni ajali, Ilowakumba na njia

 

    71.    Wakazidi kutongoa, Na qamisi kuitoa, Ilokua na madoa, Ya damu iloingia

 

    72.    Uongo walouzuwa, Walosema ndugu hawa, Yusufu ameuawa, Kwa mbwa kumrukia

 

    73.    Baba kusikia yale, Ya wanawe muda ule, Na huzuni pale pale, Alianza na kulia

 

    74.    Baba alisema kua, Kwa mwanangu yalokua, Si mbwa alomuua, Wallahi nawaapia

 

    75.    Ni uongo uso shaka, Wa kanzu kutoraruka, Hata tundu kutoboka, Na mwenyewe akalia

 

    76.    Yusufu kumdhulumu, Nawaachia Rahimu, Ndie mwenye kuhukumu, Yote Mola yamwelea

 

    77.    Sasa Yusufu Misiri, Kafika na wasafiri, Maliki akaghairi, Na Yusufu kubakia

 

    78.    Kampeleka makani, Mtume wa Rahamani, Ambapo ni mnadani, Ili kwamba kunadiwa

 

    79.    Na kwa bahati nzuri, Akatokea waziri, Kadawaa kwa uzuri, Aliopewa nabiya

 

    80.    Kamnunua Yusufu, Kwa bei ilo pungufu, Kama mtumwa dhaifu, Asiye na manufaa

 

    81.    Waziri akamtwaa, Yusufu nae kukaa, Kama mwana wa kuzaa, Mahaba yalomwingia

 

    82.    Baadae atamke, Kumwambia mke wake, Zulekha mwana mshike, Mola katujaalia

 

    83.    Waziri bila ya khofu, Akaishi na Yusufu, Asimpe taklifu, Kwa kila lenye udhia

 

    84.    Waziri akamsifu, Kwa wake uaminifu, Akimpa maalufu, Mali kuyasimamia

 

    85.    Sasa hapa tufahamu, Umri aliotimu, Ndiyo apewa ilimu, Na hikima zote pia

 

    86.    Ili kufunzwa khabari, Ya ndoto kuzibashiri, Na akawa ni hodari, Kujua mambo ya ruya

 

    87.    Hata kwa muda fulani, Hapo Zulekha nyumbani, Ndipo yuwaanza zani, Maovu kuazimia

 

    88.    Kila siku yamoyoni, Iwapo mili ya ndani, Yusufu kumtamani, Kumuwazia mabaya

 

    89.    Zulekha yalikithiri, Mapenzi kumuathiri, Na hapo akamghuri, Ibilisi kumwingia

 

    90.    Kukicha azidi huba, Vitendo vya ukahaba, Ili yake matilaba, Yapate kumnyokea

 

    91.    Tangu akipenda siri, Na mwisho asisubiri, Mambo yakawa dhahiri, Kwa huba kumtokea

 

    92.    Na siku hiyo yakini, Waziri hako nyumbani, Mumewe yusafarini, Ndipo aanza udhia

 

    93.    Na ndiyo siku hakika, Zulekha kufedheheka, Na yake kutotendeka, Aliyoyaazimia

 

    94.    Wakati ulipofika, Hiyo siku aloweka, Zulekha akatamka, Na Yusufu kusikia

 

    95.    Alimwita faraghani, Zulekha kwake chumbani, Amueleze kanuni, Hilo alokusudia

 

    96.    Yusufu akamwitika, Zulekha bibi labeka, Kwa upesi akatoka, Alikoitwa kungia

 

    97.    Hata akifika ndani, Akasubiri makini, Asikize jambo gani, Bibi alilomwitia

 

    98.    Ndipo basi atamke, Huyu baa mwanamke, Amwambie haja yake, Yusufu kumwelezea

 

    99.    Akatamka machafu, Zulekha bila kukhofu, Yusufu kumuarifu, Na nguvu kumtilia

 

    100.    Kasema kwa yake dhati, Zulekha muhasharati, Kila njia kutafiti, Amghilibu rasua

 

    101.    Akazidi ubazazi, Akanena ya upuzi, Kumpa Yusufu wazi, Lake alohitajia

 

    102.    Moyo wako burudika, Niridhi ninalotaka, Na huna la kukufika, Lolote lenye udhia

 

    103.    Yusufu hapo rasuli, Kupata hino kauli, Ilimdhuru akili, Na moyo kushitukia

 

    104.    Moyo ukabadilika, Yusufu kukasirika, Akaanza kumwepuka, Kabisa kutoridhia

 

    105.    Kasema Yusufu katu, Jambo hilo sithubutu, Sitendi yaso na utu, Ya kumuudhi Jalia

 

    106.    Basi ndipo hapo hapo, Zulekha pake alipo, Katambua yaliyopo, Yake kutomnyokea

 

    107.    Akainuka haraka, Ili kutaka mshika, Na Yusufu kaepuka, Zulekha kumkimbia

 

    108.    Zulekha kwa zake kasi, Asimshike khalisi, Ila kugwia qamisi, Muda alimtapiya

 

    109.    Alimshika kwa nyuma, Akaivuta kwa hima, Libasi ikamwandama, Qamisi kuipasua

 

    110.    Ikawa kuchoropoka, Yusufu akaokoka, Na vazi limepasuka, Wakati ajitetea

 

    111.    Zulekha uchungu wake, Kwa Yusufu amwepuke, Kapasua nguo zake, Na makucha kujitia

 

    112.    Maana ya hiki kisa, Nguo zake kuzitesa, Ilikua ni siasa, Yusufu kumchongea

 

    113.    Kusudio ni kunena, Arudipo wake bwana, Kumtilia fitina, Yusufu kumzulia

 

    114.    Ghafula mara waziri, Karudi kwenye safari, Akingia yake dari, Mlangoni kufikia

 

    115.    Ndipo kuwahi matata, Mwenyewe akayakuta, Kwa kushuhudia vita, Vya mkewe na nabiya

 

    116.    Moyowe ulishituka, Kwa mambo kubadilika, Si kama alivyotoka, Mbele ya kusafiria

 

    117.    Moyo mengi ukahisi, Khofu ndani ya nafusi, Akazidi wasi wasi, Kuona yalivyokua

 

    118.    Waziri kumtangaza, Zulekha kumueleza, Hebu bibi nieleza, Ni vipi umechukiwa

 

    119.    Niambia tafadhali, Ijapokuwa qalili, Niondowe mushikili, Zulekha bibi nambiya

 

    120.    Na Zulekha akajibu, Kwa nyingi zake ghadhabu. Kumpa mume jawabu, Kisa kilomfikia

 

    121.    Bwana unavyoniona, Wala sina la kunena, Ni mambo ajabu sana , Mtu akiyasikiya

 

    122.    Akaanza kwa mpango, Zulekha wake uongo, Kumtakia kifungo, Yusufu pasi na njia

 

    123.    Alimwambia mumewe, Yalonikumba ujuwe, Yote dhamana ni wewe, Bwana ulonitakia

 

    124.    Nimetendewa vituko, Mume wangu nawe huko, Na Yusufu mtu wako, Huyo uloniletea

 

    125.    Ni jambo la kipumbavu, La kunishika kwa nguvu, Anifanye tendo ovu, Nami nikakatalia

 

    126.    Tena akanisumbuwa, Ni lazima lake kuwa, Nguo zangu kupasuwa, Kutaka nigeukia

 

    127.    Na mara bila ajizi, Kijana kasema wazi, Mbele yao kubarizi, Na wote wakasikia

 

    128.    Kwa nguvu zake Karima, Mola mwingi wa rehema, Mwana mchanga kasema, Bila khofu kumwingia

 

    129.    Alinena hivi sasa, Sote tufanye siasa, Tutamjua mkosa, Ni yupi alokosea

 

    130.    Tuliyopo hapa sisi, Tupeleleze tukisi, Tuitazame qamisi, Kwa ilivyonyanyuliwa

 

    131.    Upande ulopasuka, Nguo hio kunyanyuka, Tutamjua hakika, Vita alotangulia

 

    132.    Na qamisi ndio ile, Nyanyuko likiwa mbele, Hapo hapana kelele, Yusufu amekosea

 

    133.    Au tukiitazama, Imepasuka kwa nyuma, Zulekha ana lawama, Na ndie mwenye khatia

 

    134.    Kijana alipokoma, Mwana mchanga kusema, Ikawa ni rai njema, Ushahidi alotoa

 

    135.    Hata walipochungua, Qamisi kuangaliwa, Nyuma imepasuliwa, Wote kuishuhudia

 

    136.    Basi kwa hichi kiwango, Tushaujua mpango, Zulekha ndie muongo, Yusufu kumzulia

 

    137.    Mwishowe kimtangaza, Wanawake kueleza, Zulekha ni miujiza, Kwa yeye kutenda haya

 

    138.    Kwani hawajaamini, Banati hao yakini, Kujua yuhali gani, Uzuri wake nabiya

 

    139.    Khalafu wakatamka, Banati wakamtaka, Ili Yusufu kufika, Wapate mshuhudia

 

    140.    Hapo Zulekha mwenyewe, Akasikia mwishowe, Kwa kumsema wenziwe, Khabari kumtokea

 

    141.    Ndipo ghera kumshika, Kwake akawaalika, Na vyakula akaweka, Wote wakahudhuria

 

    142.    Akapitisha sharuti, Mbele yao mabanati, Wakayakubali dhati, Zulekha alowambia

 

    143.    Yusufu alipopita, Banati wakamkuta, Kwa visu wakajikata, Bila ya kufahamia

 

    144.    Wote kodo macho mbele, Ajabu ya maumbile, Wakakatika vidole, Kwa urembo wa nabiya  

 

    145.    Ni hapo kujulikana, Hapo walipomuona, Kuwa ni mzuri sana, Yusufu wameridhia

 

    146.    Mwanena lawama kwangu, Kwa hasira na uchungu, Jitizameni wenzangu, Nanyi yalowafikia

 

    147.    Nanyi mumeadhirika, Kushinda yalonifika, Na vidole kukatika, Bila ya kuzingatia

 

    148.    Wakazidi kina mama, Waeleza kua kama, Zulekha hana lawama, Yusufu katimilia

 

    149.    Basi mwisho akapuza, Kwa hasira kumkaza, Zulekha kuwaeleza, Wenziwe kuwaambia

 

    150.    Yakuwa asipoweza, Yusufu kunisikiza, Nyumba yake ni gereza, Lazima ataingia

 

    151.    Namweleza ya muanga, Yangu anapoyapinga, Hakika nitamfunga, Kiapo namuapia

 

    152.    Kisha tena awambiye, Hao mabibi wenziye, Na nyinyi semeni naye, Huenda akasikia

 

    153.    Zulekha kumpa nguvu, Kwa alosema maovu, Wakafanya uerevu, Tumwa kumkazania

 

    154.    Ndipo wakamuarifu, Kwa nguvu na takilifu, Wakamwmbia Yusufu, Ya bibi yako ridhia

 

    155.    Ikawa asitamke, Yusufu asiyashike, Maneno ya wanawake, Hayo waliyomwambia

 

    156.    Kwa hayo aloambiwa, Akaona hana dawa, Ila ya kuomba dua, Kwa Mola wake Jalia   

 

    157.    Na Yusufu dua yake, Ni machafu yamwepuke, Kalingana Mola wake, Hapo akaombolea

 

    158.    Ya Rabi Mola ujuwe, Yashanishinda mwenyewe, Uiwezae ni Wewe, Shida yangu yakwelea

 

    159.    Nihifadhi Bwana Mola, Kwani sina tena hila, Kwangu kheri kwenda jela, Kuliko huno udhia

 

    160.    Mungu aliyakubali, Maombi yake rasuli, Kwa mujibu wa kauli, Ya dua yake nabiya

 

    161.    Akamkinga Jalali, Na wa Zulekha muhali, Rabi akatakabali, Na gerezani kungia

 

    162.    Ikawa si muda tena, Zulekha kungoja sana, Ndipo aanze fitina, Uongo kuuchochea

 

    163.    Maana alipojuwa, Atakalo halikuwa, Tena ameadhiriwa, Khabari zimeenea

 

    164.    Akamwambia waziri, Mume wake kasisiri, Bwana nnayo khabari, Tafadhali nisikiya

 

    165.    Nakuomba kwa hisani, Yusufu mtie ndani, Mpeleke gerezani, Kwani amenikosea

 

    166.    Mji wote ni sherehe, Yusufu kunifedhehe, Katu usimsamehe, Idhara imeenea

 

    167.    Na kwa hapo ndipo mume, Asijibu asiseme, Ya mkewe aandame, Bila ya kufikiria

 

    168.    Waziri akawa radhi, Ili bibi amridhi, Mkewe asimuudhi, Ijapo ni jambo baya

 

    169.    Kamtia kifungoni, Yusufu korokoroni, Hali hako makosani, Badili kumuonea

 

    170.    Yusufu akenda ndani, Na wawili ithinani, Walokua khatiani, Kwa yao walokosea

 

    171.    Walifanya ukhalifu, Mfalume kaarifu, Wafungwe wawe madufu, Na adabu kuwatia 

 

    172.    Kwa kutokea ubishi, Kwa ndoto za ushawishi, Waloota watumishi, Jela walikofungiwa

 

    173.    Na wakenda kwa Yusufu, Kwa shaka na takilifu, Kwani ashawaarifu, Kua ndoto zamwelea

 

    174.    Saiki ndie wa kwanza, Aliyejitanguliza, Ndoto yake kueleza, Yusufu kuisikia

 

    175.    Akasema jana kua, Nimeota kuchukua, Sinia iliyokua, Na vinywaji vimetiwa

 

    176.    Na mwendo wangu wa shime, Njiani nisisimame, Nenda kwake mfalume, Vinywaji kumwandalia

 

    177.    Yusufu akamjibu, Kama ilivyo wajibu, Kumpa njema jawabu, Ndoto kumfasiria

 

    178.    Saiki akajibiwa, Ndoto ikaaguliwa, Kifungoni kutolewa, Tumwa kumbashiria

 

    179.    Akanena langu shika, Wala usifanye shaka, Wewe jela utatoka, Kazi yako kurejea

 

    180.    Mara hapo akaruka, Mpishi akatamka, Ili hakika kutaka, Kumjaribu nabiya

 

    181.    Asifikiri ni nini, Yakamwingia kichwani, Akaanza ubishani, Kujifanya yamwelea

 

    182.    Na hapo bila kusita, Ndoto yake kufuata, Kusema aliyoota, Yote yalomfikia

 

    183.    Yusufu kabwaga shingo, Kuusikiza uongo, Upangwavyo kwa mpango, Bila ya kuona haya

 

    184.    Ewe nabii wa Mungu, Yusufu mkubwa wangu, Nimeota ndoto yangu, Nimejitweka sinia

 

    185.    Nimejitweka kichwani, Na mikate imo ndani, Naipeleka nyumbani, Kwa mkuu wa raiya

 

    186.    Nilipokuwa njiani, Kaja ndege wa angani, Kaudona siniyani, Mkate kauchukua

 

    187.    Mkate akaudona, Kabaki nimedangana, Ndipo Yusufu kanena, Ndoto kumfumbulia

 

    188.    Fasiri ya ndoto yako, Haina salama kwako, Utakatwa kichwa chako, Lazima utauwawa

 

    189.    Mpishi akaduwaa, Akawa ataataa, Ikawa hana tamaa, Kwa alivyobashiriwa

 

    190.    Akamwambia mwalimu, Yusufu bwana fahamu, Hayo nilotakalamu, Ni dhihaka nakwambia

 

    191.    Yusufu ndipo kusema, Ujuwe huna salama, Utauliwa lazima, Kama nilokwelezea

 

    192.    Siku nyingi zisitimu, Kwa rehema za Karimu, Mungu akamrehemu, Saiki kafunguliwa   

 

    193.    Mwenziwe yule laimu, Aliyengiwa na hamu, Ikatolewa hukumu, Akenda akauwawa

 

    194.    Na siku ya kuachana, Na Yusufu kuagana, Hapo Yusufu kanena, Saiki kumwashiria

 

    195.    Akamba leo watoka, Kwako nnalolitaka, Siwache kunikumbuka, Yakumbuke mazoweya

 

    196.    Ewe wangu muhisani, Sinisahau mwendani, Na kunitaja nyumbani, Kwake mfalume pia

 

    197.    Saiki kenda kuanza, Kazi yake kufanyiza, Shetani kamsauza, Kutekeleza wasia

 

    198.    Ikatukia azizi, Maliki kwenye malazi, Alipitiwa na njozi, Mno kaigutulia

 

    199.    Muda alipogutuka, Malazini kuamka, Akangiwa na wahaka, Wasiwasi kumwingia

 

    200.    Akawataka Maliki, Watumiao falaki, Watizame kisa hiki, Cha ndoto ilomjia

 

    201.    Kawaita makuhani, Wakuu wanavyuoni, Wote walio mjini, Kuja kumbashiria

 

    202.    Nimewaita wajuzi, Muifanye yangu kazi, Ya ndoto munipe wazi, Jawabu ilo na njia

 

    203.    Bidii munavyoweza, Munipe ya muangaza, Kwani yamenishangaza, Sasa nawatamkia

 

    204.    Nimeota waungwana, Usingizini kuona, N'gombe walodhofu sana, Sabaa katika ruwiya

 

    205.    Huwala walionona, N'gombe sabaa mabwana, Kisha nikaota tena, Baada ya mambo haya

 

    206.    Nikayaota mashuke, Yaso kitu ndani yake, Na mengine yalo pweke, Sabaa yaliyojaa

 

    207.    Ikabidi makuhani, Kutazama vitabuni, Kuiona hawaoni, Akili zimewashia

 

    208.    Kushindwa kwa watu hao, Maliki kazidi mwao, Akawa hana makao, Wasiwasi kuzidia

 

    209.    Saiki akagutuka, Ghafula kamkumbuka, Yusufu akatamka, Maliki kumwelezea

 

    210.    Saiki katakalamu, Kumwambia muadhamu, Mimi bwana nafahamu, Wakati nilipokuwa

 

    211.    Nimefungwa gerezani, Nilimkuta mwendani, Mfadhila na hisani, Ajuaye mambo haya

 

    212.    Na Yusufu kakariri, Bila ya kuyafikiri, Ndoto akaibashiri, Alivyombashiria

 

    213.    Ni miaka ya neema, Sabaa ya wakulima, Watavuna vuno jema, Chakula cha kuzidia

 

    214.    Ikisha miaka hiyo, Yenye shibe iso choyo, Itakuja mengineyo, Saba ya watu kulia

 

    215.    Kilio kiso nyamaa, Kwa kungiliwa na njaa, Iwe ni kuu balaa, Chakula kuwashilia

 

    216.    Kupata hayo Saiki, Mambo yakamuafiki, Akamwambia rafiki, Yusufu tuonye njia  

 

    217.    Yusufu yake kalima, Kampa jawabu njema, Nawalime wakulima, Mavuno yakiwadia

 

    218.    Mupatafute mahala, Muvitie kwenye ghala, Shida ikija ghafula, Mupate cha kutumia

 

    219.    Basi hapo ikabidi, Bwana Saiki karudi, Na kamili ushahidi, Wa kwenda kuwaridhia

 

    220.    Hata akifika ndani, Kwa mfalume nyumbani, Akaeleza makini, Yote yaliyotukia

 

    221.    Alimpa tafsiri, Ya ndoto yake dhahiri, Mambo yatakayojiri, Ambayo yatatokea

 

    222.    Papo kastaajabu, Mfalume kwa jawabu, Mno kaona ajabu, Kwa ujuzi wa nabiya

 

    223.    Na pale pale kwa hamu, Maliki katakalamu, Saiki kumlazimu, Upesi jela rejea

 

    224.    Mwite Yusufu haraka, Umwambie ukifika, Mfalume akutaka, Haraka akungojea

 

    225.    Kufika kwenye kizimba, Asingoje akamwamba, Yusufu bwana aomba, Wende kwake akwambia

 

    226.    Kukangiya walakini, Kuwa haiwezekani, La kutoka gerezani, Yusufu kakatalia

 

    227.    Akasema kumjuza, Saiki kumueleza, Mimi katika gereza, Sitaondoka sikia

 

    228.    Salamu zangu zifishe, Mfalume mjulishe, Mpaka athubutishe, Yakua sikukosea

 

    229.    Na kisha kwa hiki kisa, Awajuze watu khasa, Yakuwa sina makosa, Zulekha ndie mbaya

 

    230.    Awaite vilevile, Banati wa siku ile, Walojikata vidole, Na Zulekha wote pia

 

    231.    Ni kua apeleleze, Maliki awaulize, Wanawake wamweleze, Ni yupi alokosea

 

    232.    Saiki akaushika, Ujumbe kaupeleka, Yote aliyotamka, Yusufu kumwaridhia

 

    233.    Alipokwisha ambiwa, Maliki kuelezewa, Maneno yakamtuwa, Pingamizi kutotia

 

    234.    Ndipo hapo apeleke, Mfalume mtu wake, Wakaitwe wanawake, Na wote wakafika

 

    235.    Banati wakiwasili, Maliki kawakabili, Kisha akawasaili, Mfalume kuwambia

 

    236.    Musiogope muhali, Baina hawa wawili, Mwenye makosa kwa kweli, Mwaweza kunitajia

 

    237.    Ni Zulekha na Yusufu, Mkosa muniarifu, Yupi alo mpotofu, Huyo alo na hatia

 

    238.    Wanawake wakasema, Kwa upole na heshima, Bwana mwenye na lawama, Zulekha ndie mbaya

 

    239.    Na Zulekha baadae, Akiulizwa na yeye, Asili asikatae, Akajibu ya sharia

 

    240.    Yakua wangu ulimi, Leo uongo sisemi, Mwenye makosa ni mimi, Hakika nakubalia

 

    241.    Mfalume ufahamu, Yusufu simlaumu, Bali niememdhulumu, Na tena kumzulia

 

    242.    Zulekha akalingana, Ya Ilahi Subhana, Nakubali mimi Bwana, Yakua nimekosea

 

    243.    Na makosa kua kwangu, Nakuomba Bwana Mungu, Nisamehe dhambi zangu, Ya Rabbi Mola Jalia

 

    244.    Yote maneno ya watu, Yusufu imethubutu, Si mkosa huyu mtu, Hakika imetokea

 

    245.    Imethubutu Yusufu, Kua mtu mtukufu, Sababu hana machafu, Maovu kujizuiya

 

    246.    Zulekha alitamka, Kua alighilibika, Ndie aliemtaka, Sasa amekubalia

 

    247.    Tushafahamu Yusufu, Kwamba hana ukhalifu, Zulekha ndie mchafu, Kosa lilomwelemea

 

    248.    Alipopata ukweli, Maliki kwa jambo hili, Ikawa yastahili, Yusufu kwenda tolewa

 

    249.    Ndipo Saiki atoka, Kwa furaha na kucheka, Kwa Yusufu akifika, Akawa atmwambia

 

    250.    Itunze yako nafusi, Usiwe na wasiwasi, Zulekha ndie mkosi, Makosa ameridhia

 

    251.    Wameitwa watu tele, Kaulizwa mambo yale, Akajibu yale yale, Kama yalivyotokea

 

    252.    Yusufu iliyobaki, Sasa twende kwa Maliki, Usiwe mwenye hamaki, Kufikiri mambo haya

 

    253.    Yusufu akaitika, Gerezani akatoka, Kwa Maliki akafika, Vizuri akapokewa

 

    254.    Maliki akasimama, Mtukufu wa heshima, Akampa taadhima, Sitaha kumfanyia

 

    255.    Maliki kamkubali, Kuwa ni mtu wa kweli, Tena ni mwenye akili, Yusufu kajaaliwa

 

    256.    Yusufu akataraji, Awe waziri wa mji, Awe ni mtazamaji, Neema ikitokea

 

    257.    Mfalme karidhia, Na kumsafia nia, Akamba nakuachia, Fanya litakalofaa

 

    258.    Yusufu asighairi, Wala asitaakhiri, Akashika uwaziri, Cheo hicho kupokea

 

    259.    Ndipo yaanza neema, Chakula mji mzima, Furaha kwa wakulima, Hadi waliobakia

 

    260.    Wala vyema wakishiba, Na vyengine kwa akiba, Muda wa miaka saba, Njaa kuwaepukia

 

    261.    Kwa furaha wakakaa, Muda wa myaka sabaa, Hapo ikangia njaa, Raha kuwapungukia

 

    262.    Lakini wao hakika, Japo njaa imefika, Waliishi pasi shaka, Wakila bila udhia

 

    263.    Ila ilizidi dhiki, Kwa miji iliyobaki, Kwa majirani rafiki, Njaa ikawafikia

 

    264.    Ndipo ilipomsibu, Njaa kuu Yaakubu, Kumfikia taabu, Ya wanawe wote pia

 

    265.    Yaakubu hapo basi, Akazidi wasiwasi, Wakati alipohisi, Chakula kimeishia

 

    266.    Na baba yeye mwenyewe, Akawajuza wanawe, Kuwaambia wajuwe, Njaa ile ilongia

 

    267.    Ili kwamba wasafiri, Wende mji wa Misiri, Na wana wakakhiari, Baba kumkubalia

 

    268.    Wakenda wana ashara, Ila wa hidaashara, Hakua na msafara, Nyumbani akabakia

 

    269.    Aliebaki nyumbani, Kutokua safarini, Ni huyu Binyamini, Ndie aliesalia

 

    270.    Mwana huyu mtukufu, Na tena nawaarifu, Ni mdogo wa Yusufu, Kwa baba na mama pia

 

    271.    Basi kumi walobaki, Wakenda na yao dhiki, Kuitafuta riziki, Misiri wakafikia

 

    272.    Wakawasili vijana, Hata walipopambana, Yusufu akawaona, Kwake walipoingia

 

    273.    Walipofika ikawa, Yusufu kuwatambuwa, Na wao kutomjuwa, Yakuwa ni ndugu moya

 

    274.    Yusufu akafuliza, Na wao kuzungumza, Na hali kuwauliza, Na wao kumwelezea

 

    275.    Yusufu yakamtosha, Nduguze walompasha, Nae akayakinisha, Ni nduguze wote pia

 

    276.    Khalafu mwisho akaze, Yusufu awaeleze, Awaambie nduguze, Hao walomjilia

 

    277.    Katamka akanena, Enyi ashara vijana, Munaporejea tena, Hapa mukifikilia

 

    278.    Ndugu yenu muje nae, Aandamane na nyie, Ili hapa afikie, Nipate mshuhudia

 

    279.    Hilo hakika nawapa, Nisipomuona hapa, Na chakula sitawapa, Munachokihitajia

 

    280.    Wala musinifikie, Kwangu musikaribie, Huko huko mubakie, Sitaki washuhudia

 

    281.    Ikangia tafauti, La kusema hawapati, Ikawa kwao sharuti, Ndugu hao kurejea

 

    282.    Wakapakiliwa tweka, Za chakula walotaka, Ili wapate ondoka, Makwao kurejelea

 

    283.    Walipowasili kwao, Kufikia ndugu hao, Wakampa baba yao, Khabari ilotukia

 

    284.    Walipofungua tweka, Nyoyo ziliwapasuka, Kwa furaha kuwafika, Ya mali kuregezewa

 

    285.    Hata chakula kikisha, Ndiyo siku ikatisha, Wana kujitayarisha, Safari kuandalia

 

    286.    Baba wakamshauri, Ili wao kwa uzuri, Kwa huyo mwana saghiri, Ili wende nae pia

 

    287.    Na watoto wakasema, Kumpa baba kalima, Baba hakuna hekima, Tutakayokufanyia

 

    288.    Utupe Binyamini, Awe nasi safarini, Usiwaze asilani, Salama atarejea

 

    289.    Na baba yakamtanza, Halijui la kufanza, Akakumbuka la kwanza, La Yusufu kupotea

 

    290.    Baba alifanya khofu, Akidhania machafu, Yalomkumba Yusufu, Na huyu atatendewa

 

    291.    Khalafu akakariri, Kuwapa wana khabari, Akasema mwafikiri, Kua nitakubalia

 

    292.    Na wana yao kauli, Kumtoa mushikili, Wakasema ilo kweli, Baba yao kumwambia

 

    293.    Hakika amtakae, Ili sisi twende nae, Ni waziri asemae, Ndiyo alotwelezea

 

    294.    Kwa nyingi mno taabu, Akanena Yaakubu, Wanawe akawajibu, Kwa hilo sitaridhia

 

    295.    Hendi hadi ushahidi, Munipe kweli ahadi, Yake Ilahi Wadudi, Yakuwa atarejea

 

    296.    Na ijapo ni ajali, Jambo lisokua hili, Siwalaumu asili, Apendalo Mungu huwa

 

    297.    Na wana wote walipo, Ikawa kula kiapo, Wakasema papo hapo, Kwa Mungu kushahidia

 

    298.    Wallahi twenda na yeye, Khofu isikuingiye, Baba tutakuja nae, Mwanayo atarejea

 

    299.    Baba kwa hino ahadi, Ya ashara auladi, Moyowe uliburudi, Imani ikamwingia

 

    300.    Basi baba akaridhi, Moyo wake kuwa radhi, Mwanawe kuwakabidhi, Wanawe walosalia

 

    301.    Ndipo baba amtake, Binyamini afike, Na alipokuja kwake, Mara kamkumbatia

 

    302.    Yaakubu akanena, Na mwanawe kuagana, Kwaheri ya kuonana, Na kheri nakutakia

 

    303.    Safiri Binyamini, Kwa salama salmini, Na urudi mara thani, Kwa umri na afiya

 

    304.    Hapo muda ukajiri, Hapana tena shauri, Vijana wakasafiri, Hidaashara pamoya

 

    305.    Wakenda mara ya pili, Vijana kama awali, Kwa Yusufu kuwasili, Misiri wakafikia

 

    306.    Kuwasili ikhiwani, Yusufu kwake nyumbani, Kawapanga ithineni, Wawili chumba kimoya

 

    307.    Yusufu yake akili, Kawatenga mbalimbali, Ndugu wawili wawili, Mdogo akasalia

 

    308.    Ndipo basi masikini, Kabaki pweke mwendani, Yaani Binyamini, Hapo kaanza kulia

 

    309.    Mambo yakamtatiza, Yusufu kumshangaza, Kisha akamuuliza, Mdogowe kumwambia

 

    310.    Nieleze kwa makini, Likulizalo ni nini, Walizwa na jambo gani, Nambia nipate juwa

 

    311.    Binyamini kasema, Kwa sauti ya huruma, Kumpa yake kalima, Yusufu kumwadithia

 

    312.    Lau yuhai Yusufu, Leo mimi pasi khofu, Singepata takilifu, Kwa haya kunifikia

   

    313.    Yusufu nae kajibu, Wasemaje mahabubu, Leo ni wako sahibu, Binyamini sikia

 

    314.    Yusufu na ndugu yake, Wakangia chumba pweke, Na Yusufu  atamke, Siri hapo kuitoa

 

    315.    Kampa la burudiko, Biyamini tamko, Mimi ndie ndugu yako, Yusufu alopotea

 

    316.    Na muda ulipofika, Ndugu chakula kutaka, Ili wapate ondoka, Kwa haraka kurejea

 

    317.    Wote wakamiminiwa, Magunia kujaziwa, Bila ya kulia ngowa, Na Binyamini pia

 

    318.    Lakini gunia lake, La Yusufu ndugu yake, Yaani mdogo wake, Huyo aliyeletewa

 

    319.    Humo mwake guniani, Kwa huyo Binyamini, Kaificha pishi ndani, Yusufu kumtilia

 

    320.    Ndipo ndugu wakafisha, Safari kutayarisha, Mizigo kuipandisha, Kuwabebesha ngamia

 

    321.    Na mara kwa muda huo, Kuepuka ndugu hao, Katika safari yao, Wanjiani warejea

 

    322.    Askari nae basi, Akakimbia upesi, Akawakuta khalisi, Bado wangali na njia

 

    323.    Muda alipowapata, Asikari, kuwakuta, Kwa kelele kawaita, Mkono kuwapungia

 

    324.    Askari akanena, Kuwajulisha vijana, Nasema kwenu mabwana, Jambo nilowaitia

 

    325.    Nimeambiwa nifike, Na Maliki niwashike, Imeibwa pishi yake, Ya chakula kupimia

 

    326.    Na vijana wakafika, Kwa khofu kutetemeka, Khalafu wakatamka, Askari kumwambia

 

    327.    Twaapa kwa Mwenye enzi, Twakupa iliyo wazi, Sisi bwana sio wezi, Pishi tulowaibia

 

    328.    Yusufu kasisitiza, Mwishowe kuwauliza, Ni nini yake majaza, Pishi aliyeitwaa

 

    329.    Walipoulizwa hayo, Wakamjibu kwa payo, Jaza yake mtu huyo, Adhabu kumfikiya

 

    330.    Ikatazamwa vizuri, Kwa ndugu hao kabiri, Na ikawa asikari, Pishi hakuivumbuwa

 

    331.    Basi akawa imara, Askari kuchakura, Hadi vijana ashara, Kwenye yao magunia

 

    332.    Askari kakazana, Hata wa kumi kijana, Na pia hakuiona, Pishi kuishuhudia

 

    333.    Kuja kutizama ndani, Kwa huyo Binyamini, Humo mwake guniani, Pishi hio ikagwiwa

 

    334.    Kufika wakatongowa, Uongo wakauzuwa, Kwamba huyu hana dawa, Si mwanzo kufanya haya

 

    335.    Na huyo ndugu wa mbele, Alimwivi vile vile, Hata tembe ya mchele, Akiona huitwaa

 

    336.    Yusufu katabasamu, Moyoni katakalamu, Ni uovu ulotimu, Machoni kunizulia

 

    337.    Bwana ufanye imani, Twakuomba kwa hisani, Muwache Binyamini, Tafadhali twakwambia

 

    338.    Twaomba kwako Maliki, Na sote kutuafiki, Mmoja wetu kubaki, Badili kumfidia

 

    339.    Yusufu yake kauli, La ndugu asikubali, Kushika mtu badali, Hilo hakukubalia

 

    340.    Hapo akazidi chuki, Ndugu mkubwa hataki, Kanena mimi sitoki, Misri nitabakia

 

    341.    Kuwasili kwa mzazi, Na mema maamkuzi, Kisha lao simulizi, Baba kumuhadithia

 

    342.    Siri hawakuiziba, Wakampa wazi baba, Baba mwanao kaiba, Nasi kumshuhudia

 

    343.    Na baba yake kauli, Kajibu hili si kweli, Hilo ni yenu nakili, Ni hila mwaniletea

 

    344.    Kwa yote haya madhara, Inshalla niko imara, Mungu tanipa subira, Njema ya kuvumilia

 

    345.    Kisa hiki kumfika, Ndipo alipokumbuka, Yale ya kwanza mashaka, Ya Yusufu kupotea

 

    346.    Akanena kwa uchungu, Rudini enyi wanangu, Kwenye aridhi ya Mungu, Musiogope udhia

 

    347.    Nendeni pasi nakhofu, Musijali takilifu, Mumtafute Yusufu, Na Binyamini pamoya

 

    348.    Wakafika kwa heshima, Kwake Yusufu salama, Na wote wakainama, Hishima kumfanyia

 

    349.    Khalafu kisha waanze, Wakatamka nduguze, Yusufu wamueleze, Wanalolihitajia

 

    350.    Ewe mwingi wa fadhila, Tuna haja ya chakula, Sisi na yetu aila, Tusije kufa na njaa

 

    351.    Nasi hatuna thamani, Wala kitu mkononi, Ila ni bidhaa duni, Isiyo na manufaa

 

    352.    Yusufu kasikitika, Wazazi kawakumbuka, Machozi yakamtoka, Hawezi kuvumilia

 

    353.    Sasa ndio wapambana, Yusufu na hao wana, Maswali kujibizana, Siri Yusufu atoa

 

    354.    Yote mambo ya zamani, Ya kutupwa kisimani, Ndipo hapo yabaini, Yusufu alotendewa

 

    355.    Yusufu awaambie, Ni nani wapili yeye, Alofarikana nae, Baba alompotea

 

    356.    Ndugu wakamuarifu, Wakasema bila khofu, Jina lake ni Yusufu, Mwana aloangamia

 

    357.    Na ndugu wakatongowa, Yusufu akajibiwa, Mwana huyo kauawa, Na mbwa mwitu kuliwa

 

    358.    Yusufu akatamka, Kweli mbwa kamshika, Au nyinyi kwa hakika, Kisa mumemtendea

 

    359.    Yusufu kasema tena, Na ndugu kujibishana, Hamukufanya khiana, Kisimani kumtia

 

    360.    Na papo wakajibiwa, Na Yusufu kuambiwa, Jee aliemuuwa, Ni nyinyi wenu mmoya

 

    361.    Ndugu nao kwa upesi, Wakanena kua sisi, Tutauwaje nafusi, Bila kisa kutokea

 

    362.    Basi Yusufu kakaza, Kuzidi kuwaeleza, Yote waloyafanyiza, Mpaka kuishilia

 

    363.    Na hiyo si dhambi katu, Kwa huyo mbwa wa mwitu, Hiyo ni dhambi ya watu, Yenu mulokusudia

 

    364.    Ajabu yao ni kua, Vipi Yusufu kujua, Ni kama aliekua, Yuko na wao pamoya

 

    365.    Baadae ndipo tena, Mmoja wao vijana, Alama akaiona, Yusufu kamtambua

 

    366.    Na hapo kwa nyingi khofu, Kanena kwa takilifu, Wewe kwani ni Yusufu, Bwana hebu niambia

 

    367.    Yusufu nae haraka, Na mara akatamka, Mimi ndie pasi shaka, Yusufu alopotea

 

    368.    Ndie Yusufu wenzangu, Mimi mtume wa Mungu, Na huyu ni ndugu yangu, Aliyeniandamia

 

    369.    Akazidi kukariri, Kuwapa ndugu khabari, Hakika ukisubiri, Mja kwa kila udhia

 

    370.    Nao ndugu wakaanza, Yusufu wakamweleza, Mola amekutukuza, Kwa dhiki kuvumilia

 

    371.    Kwa hili Yusufu kuwa, Mungu akujaze sawa, Kwa uliyoyachukuwa, Mambo tulokufanyia

 

    372.    Yusufu nae kasema, Kuwajibu ndugu vyema, Leo hakuna lawama, Kwenu nyinyi ndugu pia

 

    373.    Na Mola wetu Karimu, Tawasamehe Rahimu, Ndie mwenye kurehemu, Viumbe wake Jalia

 

    374.    Kisha nae atamke, Yusufu kwa ndugu zake, Qamisi muipeleke, Nawatuma nyote pia

 

    375.    Twaeni yangu libasi, Tena haraka upesi, Mufikapo na qamisi, Kwa baba mukiingia  

 

    376.    Musimpe mkononi, Nitakavyo ikhiwani, Mumbwagie usoni, Macho yatamrudia

 

    377.    Na khalafu baadae, Murudi pamoja nae, Nyote kwangu mugurie, Pasi mtu kubakia

 

    378.    Muje na wote jamaa, Na wala kutokataa, Tuje pamoja kukaa, Hapa kwangu kuguria 

 

    379.    Walipotoka nyumbani, Kwa Yusufu ikhiwani, Wakali bado ndiani, Muda wakisafiria

 

    380.    Yaakubu mtukufu, Akasikia harufu, Ya qamisi ya Yusufu, Puani kumuingia

 

    381.    Ilokwenda kwa upepo, Muda huo hapo hapo, Kwa Yaakubu alipo, Harufu kumfikia

 

    382.    Yaakubu kabashiri, Kwa walokua hadhiri, Akawapasha khabari, Akasema kuwambiya

 

    383.    Naisikia harufu, Ya mwanangu maarufu, Al-waladi Yusufu, Fuadi alopotea

 

    384.   Jamaa wakamjibu, Kumweleza Yaakubu, Yuko wapi aloghibu, Alokufa kurejea

 

    385.    Mara kwa chache dakika, Saa kutomalizika, Hapo wana wakafika, Kwa shangwe wakatokea

 

    386.    Na mbele ya kujilisi, Ili wapate marisi, Waliibwaga qamisi,Usoni kumtupia

 

    387.    Akarejea kuona, Kama zama za ujana, Na kisha ndipo kanena, Yaakubu kutongowa

 

    388.    Kujuza wale mabwana, Mbele ya kuja vijana, Kwa harufu kushindana, Wakati wakiongea

 

    389.    Yaakubu katongowa, Mambo nnayoelewa, Najuwa musoyajuwa, Mimi sikuwaambia

 

    390.    Kwa kufupisha maneno, Mambo yakawa manono, Furaha iso mfano, Kwa baba na wana pia

 

    391.    Na hapo baba na wana, Wote kukumbatiana, Dhambi kusameheana, Wana waloyakosea

 

    392.    Ikawa baba kuhama, Wana pamoja na mama, Wakawasili salama, Kwa Yusufu kuguria

 

    393.    Kawakaribisha vyema, Aila ilomwandama, Kwa adabu na heshima, Yusufu kuwapokea

 

    394.    Furaha ikawa kuu, Wana hadi wajukuu, Si shangwe mambo makuu, Furaha kuwazidia

 

    395.    Kisha ndipo kawaweka, Wazazi wake katika, Kiti chenye mamlaka, Heshima kuwafanyia

 

    396.    Na mara baba na mama, Na wana wakaandama, Kwa furaha kuinama, Wakasujudu pamoya   

 

    397.    Walipokwisha pumuka, Kwa furaha na kucheka, Wakashukuru Rabuka, Kumhimidi Jalia

 

    398.    Na muda huo haraka, Yusufu papo kafika, Ndoto yake kakumbuka,Ya zama zilopitia

 

    399.    Akamweleza mzazi, Babake kumpa wazi, Huno ndio uwaguzi, Wa ndoto nilokwambia

 

    400.    Alizidi akinena, Wa ndoto niloiona, Katika wangu ujana, Leo yatufunukia

 

    401.    Siku leo imefisha, Ya Mola kutonyesha, Haki amehakikisha, Ilahi Pweke  Mmoya

 

    402.    Tena Ilahi Karima, Kanitendea na wema, Kuniokoa salama, Jela kunifungulia

 

    403.    Na nyinyi akawaleta, Niliko kunifuata, Mukaja mukanikuta, Kwa salama na afiya

 

    404.    Kwa uwezo wa Rabbana, Kawaleta nyinyi tena, Tukaja tukaonana, Kujumuika pamoya

 

    405.    Na mwisho wake khalafu, Mtume mwema Yusufu, Kamshukuru Latifu, Huku akiombolea

 

    406.    Ewe Bwana Mtukufu, Uliyenipa sharafu, Ufalme uso khofu, Bwana Ulotimilia

 

    407.    Ukanipa na uweza, Ndoto za kimiujiza, Uwaguzi kunifunza, Tafsiri kuzijua

 

    408.    Ewe Mwenye enzi Mungu, Ya Ilahi Mola wangu, Uloumba ulimwengu, Na ardhi zote pia

 

    409.    Ya ilahi niongowa, Nipite hali ya kuwa, Kila haki kuijuwa, Na kwako kunyenyekea

 

    410.    Njia njema nionyeshe, Na wema nilahikishe, Yaani nikutanishe, Na wetu wema Jalia  

 

    411.    Na hapo akamaliza, Yusufu aloeleza, Pasi moja kulisaza, Shukurani kutumia

 

    412.    Kwa hivyo wote wendani, Wakakutana yakini, Kama zama za zamani, Siku zilizopitia

 

    413.    Kufikia kwa Yusufu, Aila ilo tukufu, Wakaishi bila khofu, Kusahau yote pia

 

    414,    Kwa furaha wakadumu, Kwenye makao timamu, Nyoyo zikatabasamu, Hadi kuaga dunia

 

    415.    Kwa kufupisha niseme, Yusufu kawa mtume, Kapata na ufalume, Mola kumjaalia

 

    416.    Basi hapa waungwana, Yatosha niloyanena, Ya zaidi tena sina, Samahani ila haya

 

    417.    Sasa ndio nasimama, Kisa chetu kimekoma, Na dua kwake Karima, Naanza kuombolea

 

    418.    Ni wewe Mola Mmoja, Muumba wa sote waja, Itimize yetu haja, Ilahi watusikia

 

    419.    Twakuomba Ya Manani, Isilamu ikhiwani, Tuongoze kwenye dini, Imani kutuzidia

 

    420.    Tupe nguvu za nafusi, Tumshinde Ibilisi, Asiipate nafasi, Njia mbovu kututia

 

    421.    Twakuomba Ya Wadudi, Machafu yawe baidi, Na waovu mahasidi, Yao kutowanyokea

 

    422.    Ya Ilahi Ya Karimu, Tupe akili timamu, Ya dini na ya ilimu, Tushike bila udhiya

 

    423.    Tulinde tuwe wekevu, Tuyaepuke maovu, Na nyoyo ziwe na nguvu, Machafu kuyakimbia 

 

    424.    Tuepushie na dhara, Kwa dini tuwe imara, Twaiomba na sitara, Ya akhera na dunia

 

    425.    Dua ifike ulipo, Na kabuli ije papo, Utupe na njema pepo, Hiyo ulotwandalia

 

    426.    Amina Rabi amina, Amina Mola amina, Utukabalie Bwana, Kwa baraka za nabiya

 

    427.    Na hapa ninamsifu, Mola wetu Mtukufu, Mkubwa Mtakatifu, Taala Rabi Jaliya

 

    428.    Na mtume Muhammadi, Mjumbe wake Wadudi, Kila siku turadidi, Swala na salamu pia

 

    429.    Bwana Saidi Karama, Mungu takwegesha pema, Akupe na nyingi hima, Malenga usiye doa

 

    430.    Nimekisoma kitabu, Hakuna moja aibu, Yote haya ni thawabu, Uliyotuhadithia