Nasaha kwa kila Shia
Imeandikwa na Sheikh
Abubakar Jaber Al Jazaairy
Imefasiriwa na
Muhammad Faraj Salem Al Saiy
www.mawaidha.info - www.alhidaaya.com
Hii Ni Zawadi Kwa Kila Shia Mwenye
Hisia Huru – Mwenye Kufikiri – Mpenda Haki Na Kheri - Anayetaka Kujuwa Na
Kufahamu – Kwa Wote Hawa Nawapa Zawadi Hii Fupi Na Simuombi Zaidi Ya Kuwa
Ayasome Makala Haya Nikiwa Na Imani Kuwa Nitakuwa Nimempa Nasaha Njema -
Wassalaam –
Al Jazairy
Bismillah wal hamdu Lillah wa
ssalaatu wa ssalaamu alaa rasuuli Llah Nabiyyuna Muhammad wa alaa aalihi wa
sahabihi.
Wabaad – Kusema kweli mimi sikuwa nikijuwa
chochote kuhusu Madhehebu ya Kishia zaidi ya kuwa wao ni watu wanaowapenda Ahli
l Bayt, na kwamba wao ni Waislamu wanaovuka mipaka katika kuwapenda watu wa
nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Ahli l Bayt’,
wanawanusuru, na kwamba hitilafu baina yao na Masunni ‘Ahli Sunnah’ ni
ndogo sana, nayo ni katika mambo yanayohusu sharia na kwamba wao huzifasiri
vibaya tu baadhi ya aya na baadhi ya hadithi za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam).
Kwa ajili hiyo, nilikuwa nikighadhibika sana pale ninapowaona baadhi ya Masunni wakiwataja Mashia
kuwa ni Mafasiq, au pale ninapowasikia wakiwatoa katika itikadi za Kiislam. Fikra zangu hizi hazikudumu muda mrefu. Mmoja katika ndugu
zangu aliponishauri nisome kitabu cha jamaa hawa (Mashia) ili
niweze kutoka hukmu yangu kwa ukamilifu na usahihi juu ya Itikadi ya Kishia.
Akanishauri nikisome kitabu kiitwacho Al Kaafi, na
hiki ni kitabu kitukufu sana kwao chenye kuyathibitisha madhehebu yao.
Nikakisoma na kupata
ndani yake ukweli wa kitaalamu ulionifanya niwape udhuru wote waliokuwa
wakinikosowa kwa kuwaunga mkono kwangu wenye kufuata Madhehebu ya Kishia. Kwani
nilikuwa nikitegemea kuwa huenda nikaweza kuziondoa baadhi ya chuki zilizopo
baina ya Ahli Ssunah na kundi hili linalojinasibisha
na Uislam kwa haki au kwa batil.
Na leo nakuleteeni
uhakika nilioupata kutoka katika kitabu chao muhimu sana wanachokitegemea
katika kuyathibitisha Madhehebu yao nikimuomba kila mwenye kufuata Madhehebu ya
Kishia asome na atafakari juu ya ukweli huu kwa ikhlas na uadililifu, kisha
atoe uamuzi wake juu ya Madhehebu yake na juu ya kujinasibisha kwake nayo. Ajiamulie mwenyewe. Iwapo atatowa hukumu kuwa Madhehebu yake
haya ni sawa na kwamba kujinasibisha kwake na Madhehebu haya ni haki na kwamba
ni bora, basi na aendelee nayo, ama iwapo atatambua ubatilifu wa Madhehebu yake
basi itampasa kila Mwenye kufuata Madhehebu haya ya Kishia ainasihi nafsi yake
na kumuomba Mola wake amsaidie katika kuyaacha, na yamtosheleze yale
yanayowatosheleza mamilioni ya Waislam ulimwenguni kote, nayo ni Kitabu cha
Mwenyezi Mungu (Qur-aan) na Mafundisho sahihi ya Mtume wake (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi w sallam).
Kisha mimi najikinga kwa Mwenyezi Mungu
kutokana na kila Muislam utakayembainikia ukweli, kisha akauacha na kuifuata
batili kwa jeuri tu, au kwa kuiga au kwa ajili ya ukabila au utaifa kwa kutaka
manufaa ya kidunia, huku akiighushi nafsi yake na kuipeleka katika njia ya
unafiki na kujihadaa, akiwa ni mtihani kwa wanawe na ndugu zake na vizazi
vitakavokuja baadaye, wote hao atakuwa amewaondoa katika njia ya haki kwa ajili
ya kufuata batili yake na kuwabaidisha mbali na Mafundisho ya Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwatia katika Uzushi na kutoka katika
Uislam sahihi na kuwaingiza katika Madhehebu maovu.
Ewe Mwenye kufuata Madhehebu ya Kishia, upokee
ukweli huu wa kitaalamu juu ya asili ya Madhehebu yako
yaliyowekwa na mikono miovu kabla yako na nafsi zilizojaa shari ili uwe mbali
kabisa na Uislam wa kweli na Haki.
Pokea ewe Mfuasi wa
Madhehebu ya Shia mafungu saba ya ukweli yaliyohifadhiwa ndani ya kitabu cha Al
Kaafi, kitabu kinachotegemewa katika kuyathibitisha Madhehebu yako na ambacho
ni chimbuko la Ushia wako. Kitazame vizuri, tafakari vizuri na
umuombe Mola wako Mtukufu akuonyeshe ukweli na akusaidie katika kuufuata na
akuwezeshe kuubeba, kwani hapana Mola isipokuwa Yeye na hakuna Muweza isipokuwa
Yeye.
Ahli L Bayti Hawaihitajii Qur-Aan
Kwa Sababu Wana Vitabu Vya Mwenyezi Mungu Vilivyotangulia Kuteremshwa, Navyo Ni
Taurati Na Injili
Ukweli huu unathibitishwa na
yale yaliyoandikwa katika kitabu cha Al Kaafi Juzuu ya kwanza Kitabul Hojjah
ukurasa wa 207, nayo ni haya yafuatayo;
((Mlango wa Maimam
Alayhimu Salaam wanavyo vitabu vyote vilivyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu
na kwamba wao wanavijua vyote, juu ya kuhitilafiana kwa lugha zake)).
Ushahidi aloutegemea mwenye kitabu cha Al Kaafi
ni hadithi mbili zilizosimuliwa na Abi Abdullahi
kwamba yeye alikuwa akivisoma vitabu vya Taurati na Injili na Zaburi kwa lugha
ya kisiri.
Na maana ya maneno haya yaliyomo ndani ya
kitabu chao hicho ni maarufu, nayo ni kuwa Maimam wao
na wafuasi wao hawana lazima ya kushikamana na Qur-aan l Karim kutokana na
wanayoyajua katika vitabu vilivyotangulia. Hii ni
hatua kubwa inayowatenga Mashia mbali na Uislam na Waislam, kwa sababu bila
shaka yoyote ile, yeyote anayeamini kuwa hana lazima ya kuifuata Qur-aan kwa
njia yoyote ile anakuwa keshatoka katika dini ya Kiislam na keshateleza mbali
na ndugu zake Waislam. Kwani Qur-aan ndiyo inayowaunganisha umma huu wa Kiislam katika itikadi zake na hukmu zake na adabu zake
na kuwafanya wawe Umma mmoja.
Si katika kuiacha Qur-aan, pale mtu anapoiacha
kuisoma na badala yake akavifuatilia na kuvidurusu
vitabu vilivyotangulia vilviyobadilishwa na kupotoshwa?
Kutojilazimisha kushikamana na
Qur-aan si Kufru hiyo na kuukimbia Uislam? Vipi inajuzu kuvisoma vitabu vile
vilivyobadilishwa na kupotoshwa wakati Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuona ''Umar(Radhiya Allaahu 'anhu)
akiwa na karatasi zilizoandikwa maandishi ya Taurati, alimnyang’anya na
kumwambia;
“Kwani
sikukuleteeni (kitabu) cheupe kisafi?”
Ikiwa Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuridhika pale alipomuona ''Umar(Radhiya
Allaahu 'anhu) akizitazama karatasi tu za Taurati – Inaingia akilini kweli kuwa
yeyote katika Ahli l Bayti waliotahirika kuwa amevijumuisha vitabu vyote hivyo
vya kale na kuvidurusu kwa lugha zake tofauti na kuiacha Qur-aan? Na kwa nini kwa ajili gani?
Allahumma wote huo ni uwongo mtupu waliowazulia
watu wa nyumba ya Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) kwa ajili ya kuupiga vita Uislam na Waislam.
Na mwisho, kila Shia inampasa kutambua kuwa
kutokuwa na haja ya Qur-aan l Karim, kitabu cha
Mwenyezi Mungu alichokihifadhi ndani ya vifua vya Waislam, kitabu kilichopo
mikononi mwao (Waislam) ambacho halijapungua ndani yake hata neno moja wala
kuzidishwa na wala haiwezekani hivyo abadan (kuzidishwa wala kupunguzwa), kwa
sababu Mwenyezi Mungu amekwishatoa ahadi ya kukihifadhi kitabu hiki pale
aliposema;
“Inna nah-nu nazzalna dhikraa wainnaa lahu lahaafidhun”
“Hakika Sisi ndio
tulioteremsha mauidha haya (hii Qur-aan) na hakika Sisi ndio tutakayoyalinda”.
Suratul Hijr – 9
Na kwamba Qur-aan ipo vile vile kama
ilivyoteremshwa na Jibril mwaminifu kwa Bwana wa Mitume yote, ipo vile vile
kama alivyoisoma Mtume wa Mwenyezi Mungu(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) na wakaisoma maelfu ya Masahaba wake(Radhiya Allaahu 'anhu) na
wakaisoma waliokuja baada yao miongoni mwa mamilioni ya Waislam kwa wingi mpaka
wakati wetu huu.
Mtu yeyote anapoitakidi kuwa hana lazima ya
kuifuata yote au hata baadhi yake kwa njia yoyote ile
anakuwa kesha rtaddi (keshatoka katika dini ya Kiislam). Mtu wa
aina hiyo habaki kuwa na sehemu yoyote ya Usilamu au ya Waislamu
Kuitakidi Kuwa Hapana Sahaba Yeyote
Aliyewahi Kuikusanya Au Kuihifadhi Qur-Aan Tukufu Isipokuwa Ali Na Maimam Wa
Ahli L Bayt (Radhiya Allaahu 'Anhu) Peke Yao.
“Nimemsikia Aba Jaafar alayhi ssalaam akisema;
“Yeyote atakayejidai kuwa eti ameihifadhi Qur-aan
yote, basi huyo ni mwongo, kwani hapana aliyeikusanya
na kuihifadhi kama ilivyoteremshwa isipokuwa Ali bin Abi Talib na Maimam
waliokuja baada yake".
Lazima utambue ewe unayefuata madhehebu ya
Shia, namuomba Mwenyezi Mungu aniongoze mimi na akuongoze wewe katika haki na
katika njia yake iliyonyooka kuwa; Itikadi kama hii, nayo ni kuwa hapana mtu
aliyewahi kuikusanya Qur-aan na kuihifadhi isipokuwa watu wa Ahli l Bayti na
wafuasi wao tu, ni ufisadi na shari kubwa sana, tunamuomba Mwenyezi Mungu atuepushe
nayo. Shari hii inamaanisha yafuatayo;
1- Kumkadhibisha
kila aliyesema kuwa ameihifadhi Qur-aan, kama vile 'Uthmaan na Ubay bin Kaab na
Zeid bin Thabit na Abdillahi bin Masaood(Radhiya Allaahu 'anhu) na wengineo
katika Masahaba wa Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambao
idadi yao ni kwa mamia. Huko ni kuwakadhibisha wote
hao na kuuondoa uadilifu wao. Maneno kama haya hayawezi kabisa kutamkwa na watu
wa Ahli l Bayti waliotahirika, bali yanasemwa na maadui wa Uislam na wanaopinga
Uislam kwa ajili ya uhasama na kuufarikisha umma.
2- Itikadi hii inaleta maana kuwa Waislam wote
wamepotoka isipokuwa Mashia wa Ahli l Bayti tu peke yao, kwa sababu yeyote
atakayeifanyia kazi Qur-aan nusu nusu bila ya ukamilifu atakuwa ametenda kitendo
cha ukafiri na upotevu kwa sababu hatokuwa amemuabudu Mola wake kwa ukamilifu,
kwani huenda hiyo sehemu ya Qur-aan isiyowafikia Waislam, ikawa imebeba
baadhi ya itikadi, ibada, mwenendo, na hukmu.
Itikadi hii pia
inaikadhibisha kauli ya Mwenyezi Mungu pale aliposema;
“Inna nah-nu nazzalna dhikraa wainnaa
lahu lahaafidhun”
“Hakika Sisi ndio
tulioteremsha mauidha haya (hii Qur-aan) na hakika Sisi ndio tutakayoyalinda”.
Suratul Hijr – 9
Na kuikadhibisha kauli ya Mwenyezi Mungu ni
kufru, na kufru kubwa iliyoje?
3 Je! Inajuzu kwa Ahli l Bayti kujihusisha peke yao na kitabu cha Mwenyezi
Mungu bila ya kuwahusisha Waislam wengine isipokuwa wale wanaowataka tu
miongini mwa Mashia wao? Je! Huku si katika kutowashirikisha Waislam wenzao
katika kufaidika na Rehma ya Mwenyezi Mungu na kuiteka
nyara?
Ewe Mola wetu
sisi tunaelewa kuwa watu wa nyumba ya Mtume wako
hawamo katika hatia hii ya uwongo huu na umlani kila anayesema uongo juu yao.
Ewe mwenye kufuata Madhehebu haya ya Kishia,
uongo kama huu hata mwendawazimu hawezi kuukubali,
sembuse wewe unayejinasibisha na Uislam na Waislam. Mtume(SA) hakufa ila baada
ya Mwenyezi Mungu kukamilisha kukiteremsha kitabu chake na baada ya
kukibainisha na kuwahifadhisha Waislam vifuani pao na kukiandika na kukieneza
baina yao, kila mtu, na Ahli l Bayti na Waislamu wenzao, wote sawa sawa hakuna
hitilafu baina yao. Na anayedai kinyume cha hivyo basi huyo
amesema uongo.
Unaonaje huyu aliyeandika maneno haya,
akitakiwa kutuonyesha hiyo Qur-aan waliohusishwa nayo Ahli l Bayti atakuwa na msimamo gani? Subhanaka Llahumma – huu ni
uongo mkubwa kabisa.
Kuhusishwa Ahli L Bayti Na Wafuasi
Wao Tu Kwa Baadhi Ya Miujiza Ya Mitume Kama Vile Jiwe Na Fimbo
Kutoka kwa Abi Basiyr,
kutoka kwa Jaafar alayhi ssalaam amesema;
“Usiku mmoja wa kiza alitoka Amiri l Muuminina
huku akisema;
"Hamhamah – hamhamah, na
usiku wa kiza, amekutokeeni Imam akiwa na nguo ya Adam na mkononi mwake ana
pete ya Suleiman na fimbo ya Musa!!!”
Na imeandikwa ndani ya kitabu hicho pia katika
Juzuu ya kwanza Kitabu cha Al Hojjah, ukurasa wa 227
kuwa; “Kutoka kwa Abi Hamza, kutoka kwa Abi Abdillahi – alayhi ssalaam kuwa
nimemsikia akisema;
“Mbao za Musa zipo kwetu na
fimbo ya Musa ipo kwetu na sisi ndio warithi wa Mitume!!!"
Baada ya haya ewe mwenye kufuata Madhehebu ya
KiShia, ujuwe kuwa itikadi hii kwa hakika inakufanya
uingie katika mambo ya ufisadi mkubwa kabisa na uovu, na wewe ukiwa ni mwenye
akili timamu huna budi kujitenga nayo na kuyakanusha. Nayo ni;
1- Kumkadhibisha Ali(Radhiya Allaahu 'anhu) – kwani Ali(Radhiya Allaahu
'anhu) alipoulizwa;
“Je Mtume wa
Mwenyezi Mungu(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) amekuhusisheni Ahli l Bayt kwa lolote (peke yenu)?”
Akasema;
“La –
isipokuwa kilichomo ndani ya ala ya upanga wangu huu”.
Akatoa karatasi
iliyoandikwa ndani yake mambo manne yaliyotajwa na
maulamaa wa hadithi kama vile Bukhari na Muslim.
2 Mwenye
itikadi hii anakuwa amemkadhibisha na kumdharaulisha
Ali (Radhiya Allaahu 'anhu) na ni dalili iliyowazi ya ujinga wa fahamu yake na
upungufu wa akili zake na kutoiheshimu nafsi yake. Kwani iwapo mtu huyu
ataulizwa;
'Iwapi hiyo pete na iwapi hiyo fimbo na ziwapi mbao (za Nabi Musa)',
angeshindwa kujibu na asingeweza kuleta chochote kati ya vitu hivyo, na kwa
ajili hii unabainika uongo wa kisa hiki mwanzo wake mpaka mwisho wake.
Na lilio wazi
kuliko hilo, ukimuuliza anayeamini hivyo;
'Kwa nini basi
Aali Bayti wasiitumie miujiza hiyo ya fimbo na pete
katika kuwaangamiza maadui wao na kuwamaliza kwani wao wamepata tabu sana
kutokana na shari nyingi walizotendewa.
Lengo la uongo huu ni kujaribu kuthibitisha
kuongoka kwa Mashia na kupotoka kwa wasiokuwa wao katika Waislam, ili kuyafanya
Madhehebu ya Kishia kubaki peke yake nje ya mwili wa Waislam na ili wahakikishe
viongozi wao na wale waliojificha nyuma yao, wenye nia ovu na tamaa wapate kile
wanachokitaka bila kujali kuwa wanaubomoa Uislam na kuuvunja umoja wa Waislam.
Na iwapo itikadi hii inaleta ufisadi na shari kama hii, basi ni itikadi ovu ilioje na ubaya
ulioje wa mweye kuwa na itikadi hii au mwenye kuridhika nayo.
Itikadi Kuwa Ahli L Bayt Na Wafuasi
Wao Wana Elimu Ya Mitume Na Ya Mwenyezi Mungu Wasiokuwa Nayo Waislam Wengine
Uhakika huu umeelezwa katika kitabu cha Al
Kaafi Juzuu ya kwanza kitabu cha Al Hojjah Ukurasa wa
138, pale aliposema;
“Kutoka kwa Abi Basiyr amesema; ‘ Niliingia kwa
Abi Abdullah alayhi Salaam, nikamwambia; Nimejitolea mhanga kwa ajili yako,
wafuasi wako wanasema kuwa Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
amemfundisha Ali Alayhi Ssalaam milango elfu ya elimu inayofungua milango elfu
mingine’, Akasema;
"Ewe Aba Muhammad,
Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amemfundisha Ali
Alayhi Ssalaam, milango elfu ya elimu, na kila mlango unafungua milango elfu
mingine’. Akasema, nikamuuliza;
"Hii kwa
ile?"
Akasema;
"Ewe Aba
Muhammad! Sisi pia tunayo Al Jaamiah na
kipi kinachokujulisha ukaijuwa hii Al Jaamiah?" Akaendela kusema; “ (Huu) ni ukurasa, urefu wake dhiraa sabini kwa dhiraa ya
Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimsomea kwa mdomo wake na huku
(Ali) akiandika kwa mkono wake wa kulia yote yaliyohalalishwa na
yaliyoharamishwa na kila kinachohitajiwa na wanadamu hata uchokozi na
kujichuna".
Nikamwambia;
“Nakwambia; 'hii
ndiyo elimu ya kweli”.
Akasema;
“Hakika hii ni
elimu na si ile. Kisha akanyamaza muda kidogo, kisha akasema;
“Tunayo pia Al Jafar (maandishi ya siri) na kipi kitakachokujulisha ukaijuwa hiyo Al Jafar? Hiki ni Chombo kilichotoka kwa Adam, ndani yake mna elimu
ya Mitume na ya waliousiwa na elimu ya Maulamaa waliotangulia wa Bani Israil”.
Nikamwambia;
“Hii ndiyo elimu ya kweli”
Akasema; Hii ni elimu
ya kweli na si ile, kisha akanyamaza muda, kisha akasema;
“Na kwetu pia tunao Msahafu wa
Fatima Alayha Salaam, wanaujuwaje wao msahafu wa Fatima?”
Nikamuuliza;
“Ni kitu gani hiki kinachoitwa msahafu wa Fatima?”
Akasema;
“Msahafu, ndani yake mna mfano wa Qur-aan yenu hii mara tatu! Wallahi
hamna ndani yake yaliyomo ndani ya Qur-aan yenu hii hata herufi moja”.
Nikamwambia;
“Na elimu ni ya
Mwenyezi Mungu”
Akanambia;
“Sisi kwetu tunayo elimu ya yaliyotangulia na
yanayotokea na yatakayotokea mpaka siku ya Kiama !!!!!!!!!!”
Ameyatamka haya kama
yalivyoandikwa.
Itikadi batili hii inaleta natija ifuatayo;
1- Kutokuwa na haja ya kitabu cha Mweyezi Mungu, na
hii ni kufru.
2- Kuwahusisha Ahli l Bayt kuwa wana elimu na ujuzi
wasiokuwa nao Waislam wenzao. Na hii inaleta maana ya kumtuhumu Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa
ameifanya hiyana elimu aliyopewa. Na bila shaka kumtuhumu Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amefanya hiyana, ni kufru.
3- Kumkadhibisha Ali(Radhiya Allaahu 'anhu). Kwani
katika hadithi sahihi, Ali(Radhiya Allaahu 'anhu)
alikwishasema;
“Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
hajatuhushisha sisi Ahli l Bayti na chochote”.
Na kumsingizia
uwongo Ali(Radhiya Allaahu 'anhu) ni haramu kama
ilivyokuwa haramu kumsingizia uwongo mtu yeyote yule.
4- Kumsingizia uwongo Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam). Na hili ni katika makosa makubwa kabisa, kwani Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema;
“Kunisingizia
uongo mimi ni tofauti na kumsingizia uwongo mmoja kati
yenu. Atakayenisingizia uongo kusudi, ataingia Motoni”.
5- Kumsingizia uongo Fatima(Radhiya Allaahu 'anhu)
kuwa eti ana Msahafu wake mkubwa kuliko Qur-aan mara tatu, na kwamba hamna
ndani yake katika maandishi ya Qur-aan hata herufi moja.
Mwenye itikadi
hii hawezi kuwa Muislam, au kuhesabiwa kuwa ni mmoja
wao, wakati yeye anaishi katika elimu na uongofu wasiokuwa nao Waislam wenzake.
6- Na
mwisho, Je! Uzushi huu na batili hii na uongo huu wa
kipuuzi unasihi kunasibishwa na Uislam, dini ya Mwenyezi Mungu ambaye haikubali
dini nyingine isipokuwa hii?
((Na anayetaka
dini isiyokuwa ya Kiislam basi haitakubaliwa kwake. Naye Akhera
atakuwa katika wenye khasara (kubwa kabisa))) Aali Imran - 85
Kwa ajili hiyo ewe Mwenye kufuata Madhehebu ya
Kishia, ili tuokoke na tatizo hili kubwa, sema pamoja
nami;
“Mola wangu mimi nakukanushia yale
waliyokusingizia waongo hawa, Wewe pamoja na Mtume wako na Ahli Bayti yake
waliotahirika, kwa ajili ya kuwapotosha waja wako na kuifisidi dini yako na
kuuvuruga umma wako Umma wa Mtume wako(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam).
Itikadi Kuwa Musa Kadhim Amjitolea
Mhanga Kwa Ajili Ya Kuwaokoa Mashia
Mwandishi wa kitabu
cha Al Kaafi ameandika katika kitabu hicho katika Juzuu ya kwanza kitabu cha Al
Hojjah, Ukurasa wa 260 kuwa;
Hakika Abal Hassan Kadhim (huyu ni Imam wa saba katika maimam wa madhehebu ya Ithnaasheri)
amesema;
“Mwenyezi Mungu Azza wa
Jallah alighadhibika na Mashia akanitaka nichague ama mimi ama wao, na mimi
nikakubali kuwakinga kwa nafsi yangu”.
Sasa ewe ndugu
yangu unayefuata Madhehebu ya Kishia, hebu nambie; Kisa hiki wanachokutaka wewe
ukiamini kinataka kutufundisha kitu gani?
Maana ya kisa hiki ni
kuwa;
Musa Kadhim, Mwenyezi Mungu amrehemu,
amejitolea mhanga kufa yeye kwa ajili ya kuwaokoa
wafuasi wake ili Mwenyezi Mungu awaghufurie na kuwaingiza Peponi bila
kuhesabiwa. Jaribu kutafakari ewe unayefuata Madhehebu ya Kishia – Namuomba
Mwenyezi Mungu aniongoze mimi na wewe katika yale
anayoyapenda na kuridhika nayo katika itikadi na maneno na matendo mema. Hebu
tafakari juu ya uwongo huu, kwani huu bila shaka ni
uwongo ulio mbali kabisa na haki na ukweli.
Ukiutafakari
uongo huu utajikuta unalazimika kuitakidi mambo makubwa mengi usiyopenda wewe
mwenyewe kunasibishwa nayo wala kujinasibisha nayo, nayo ni haya yafuatayo;
1- Kumsingizia uongo Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa
eti amemfunulia Wahyi Musa bin Kadhim kwamba eti ameghadhibika na Mashia na
kwamba Musa bin Kadhim amejitolea nafsi yake mhanga kwa ajili ya kuwaokoa
Mashia. Huu Wallahi ni uongo aliosingiziwa Mwenyezi
Mungu anayesema katika Qur-aan;
((Na nani dhalimu
zaidi kuliko yule aliyemsingizia uongo Mwenyezi Mungu)) [Al-An'aam: 21]
Na nani
dhaalimu zaidi kuliko anaye mzulia uwongo Mwenyezi Mungu
2-
Kumsingizia uongo Musa Al Kadhim Mwenyezi Mungu amrehemu, ambaye Wallahi si
Mtume (si Rasul wala Nabiy) na hii kauli aliyosingiziwa
kuwa eti amesema kuwa;
“Mwenyezi Mungu
Azza wa Jallah alighadhibika na Mashia akanitaka
nichague ama mimi ama wao, na mimi nikakubali kuwakinga kwa nafsi yangu”.
Kauli hii ya
kuridhika kujitolea mhanga kwa ajili ya Mashia ni
dalili ya kusingiziwa utume huyu Musa bin Khadhim (Rahimahu Llah)!!!!! Wakati
katika itikadi ya Kiislam, mtu kuitakidi kuwa yupo mtume baada ya Muhammad(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni
kufru, kwa sababu huku ni kuikadhibisha kauli ya Mwenyezi Mungu pale aliposema;
((“Muhammad si
baba wa yoyote katika wanaume wenu, bali yeye ni Mtume
wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Mitume.”)) Al Ahzab - 40
3-
Itikadi ya Madhehebu ya KiShia kukubaliana na itikadi ya Manasara juu ya kusulubiwa na kutolewa mhanga,
kwani Manasara wanaitakidi kuwa Issa (AS) amejitolea mhanga nafsi yake kwa
ajili ya kuwaokoa wanadamu kutokana na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu juu yao. Na
Mashia wanaitakidi hivyo hivyo kuwa Musa Al
Kadhim alishauriwa na Mola wake iwapo anahiari Mashia waangamizwe au afe yeye,
akakubali afe yeye ili awaokowe Mashia wake na kuwakinga na ghadhabu ya
Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo Mashia na Manasara itikadi
yao ni moja na Manasara ni makafiri kama ilivyoandikwa katika kitabu cha
Mwenyezi Mungu. Je! Mwenye kufuata madhehebu ya Kishia yuko radhi naye awe kafiri?
Mwisho nakuomba uiokowe nafsi yako ewe mwenye
kufuata Madhehebu ya Kishia na uikanushe batili hii,
na mbele yako ipo njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyoka, njia ya Waislam.
Kuitakidi Kuwa Maimam Wa Mashia,
Daraja Lao Ni Sawa Na Daraja La Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa
Sallam) Katika Kukingwa Wasifanye Madhambi Wala Makosa Na Pia Katika Kufunuliwa
Wahyi Na Katika Kutiiwa (Ta-A) Na Mengine . Isipokuwa Katika Kuowa, Wao
Hawaruhusiwi Kuowa Kama Alivyoruhusiwa Mtume(Swalla
Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam).
Itikadi hii inayowapandisha Maima wa Kishia kuifikia daraja ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam), imeandikwa na kuthibitishwa na mwandishi wa kitabu cha Al
Kafi kwa kuegemea ushahidi wake kutoka katika riwaya mbili.
YA KWANZA; Hadithi iliyosimuliwa katika
((kitabu cha Al Hojjah - ukurasa wa 229)); pale
aliposema;
"Al Mufadhal alikuwa kwa Abu Abdullah
akamuuliza;
"Nimejitolea
mhanga kwa ajili yako, ni kweli kuwa Mwenyezi Mungu anaweza kuwafaridhishia
watu kumtii mtu kisha akamzuilia mtu huyo kheri itokayo mbinguni?
Abu Abdillahi (katika maimam wa
Mashia) akamjibu;
"La- Mwenyezi Mungu ni
Mkarimu na Mwenye Huruma na Mpole zaidi kwa waja Wake, hawezi kuwafaridhishia
waja wake kumtii mtu, kisha amzuwilie mtu huyo kheri itokayo mbinguni asubuhi
na jioni".
Maneno ya riwaya hizi yanatujulisha kuwa
(kutokana na itikadi za Kishia) watu wamefaridhishiwa kuwatii maimam asubuhi na
jioni, kwa amri itokayo mbinguni na kwamba kuwatii huko kuwe kwa ukamilifu usio
na mipaka mfano wa taa-a tulivyoamrIshwa kumtii Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na kwamba Maimam hao wa Kishia wanafunuliwa
wahyi na kwamba wanapata habari kutoka mbinguni asubuhi na jioni, na kwa ajili
hiyo wao na Mitume (Anbiyaa na Mursaliyn) ni sawa sawa hapana tofauti yoyote
baina yao.
Kuitakidi kuwa yupo anayefunuliwa Wahyi baada
ya Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
ni kurtadi kutoka katika dini ya Kiislam na ni kufru, na jambo hili maulamaa
wote wamekubaliana bila hitilafu yoyote baina yao.
SubhaanaLlah vipi mwenye kufuata madhehebu ya
Kishia anakubali kutungiwa uwongo na kulazimika
kuukubali huku akiishi mbali kabisa na Uislam wa kweli akiitakidi itikadi za
kikafir wakati nia yake ilikuwa ni kuitakidi itikadi za Kiislam kwa ajili ya
kufuzu ili awe mmoja wao.
Mwenyezi Mungu ukate mkono wa muovu wa mwanzo
aliyewaweka mbali Nawe na kuwatenga mbali na njia yako .
YA PILI; Hadithi iliyosimuliwa katika ((Juzuu
ya kwanza ya kitabu cha Al Hojjah - ukurasa wa 229)).
Amesema;
'Kutoka kwa Muhammad bin Salem, amesema;
"Nimemsikia Aba Abdullah alayhi Ssalaam akisema;
"Maimamu daraja lao ni sawa na daraja la Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), isipokuwa
wao si Mitume na hawaruhusiwi kuowa kama alivyoruhusiwa Mtume(Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam). Ama kwa mengine yasiyokuwa hayo, daraja lao ni
sawa na la Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam)".
_____________
Riwaya hizi, ingawaje kwa dhahiri yake
zinaonesha kama kila moja inaikanusha nyengine, lakini undani wake ni sawa na
riwaya zilizotangulia zinazothibitisha kukingwa kwa maimamu hao wasifanye
madhambi na pia kuwajibika kuwatii na kwamba wanafunuliwa wahyi, kwa sababu
daraja ya Imam kwao wao ni daraja lililo sawa na daraja la Mtume(Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam), isipokuwa katika kuowa TU, na kwamba wao
wamekingwa na Mwenyezi Mungu wasifanye kitendo chochote cha dhambi, pamoja na
kuwajibika kuwatii na kwamba wamehusishwa na kila alohusishwa Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukamilifu.
Kusudi la kweli la uongo huu ewe mwenye kufuata
Madhehebu ya Kishia ni kutaka kuufarikisha umma wa Kishia na Uislam, ili kupiga
vita kwa hoja kuwa eti umma wa Kishia hawana haja na kile walicho nacho Waislam
katika Wahyi wa Kitabu kitukufu na Uongofu wa Mafundisho ya Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwa sababu wao wanao Msahafu wa
Fatima(Radhiya Allaahu 'anhu) ambao ni bora kuliko Qur-aan tukufu na maandishi
ya siri yaliyokusanya ndani yake elimu zote pamoja elimu ya Mitume
iliyotangulia na kwamba Maimam waliokingwa wanafunuliwa kama Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akifunuliwa isipokuwa katika
masaala ya kuowa zaidi ya wake wanne na mengine yaliyo na mfano huo yanayowatoa
Mashia nje ya Uislam kama unywele unavyotolewa ndani ya unga uliokandwa
Tunamuomba Mwenyezi Mungu aikate roho ya shari iliyoukata mwili huu mpenzi kutoka katika mwili wa
Umma wa Kiislam kwa jina la Uislam na kuwabaidisha viumbe wengi kwa kutumia
njia ya Aali Bayti, kwa mwito wa kuwanusuru Ahli l Bayti.
Kuitakidi Kuwa Masahaba Wa Mtume
(Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Wote (Radhiya Allaahu 'Anhu)
Wamertaddi Na Kukufuru Baada Ya Kufa Kwake Isipokuwa Ahli L Bayti Na Wengine
Wachache Kama Vile Salman Na Ammar Na Bilal (Radhiya Allaahu 'Anhu)
Hii ni itikadi
inayokubaliwa na karibu wanavyuoni wote wakubwa wa Madhehebu ya Kishia, na kwa
ajili hiyo vitabu vyao vyote vinazungumza juu ya maudhui hayo. Kutokutangaza
kwao rasmi katika vyombo vya habari ni kwa ajili ya
itikadi yao nyingine iitwayo 'Taqiya' (kutokusema ukweli), itikadi hii ni
wajibu katika Madhehebu yao.
Ama ushahidi wa ukweli huu na ili kuupata uhakika wake, tunakuleteeni
dalili zifuatazo;
1- Katika kitabu
cha Roudhatul Kaafi cha Al Kilaniy mwenye kitabu hiki cha Al Kaafi, ukurasa wa
202 anasema;
"Kutoka kwa Hanan kutoka kwa Abi Jaafar
amesema;
"Hao (wasiokufuru peke yao) ni Mikidadi,
Suleiman na Aba Dhar."
Katika Tafsiri ya Al Saafi - na hii ni Tafsiri
maarufu sana na inayoheshimiwa sana katika Madhehebu ya Kishia na
inayotambulika zaidi, zimo ndani yake riwaya nyingi sana zinayoitilia nguvu
itikadi hii ya kuwa Masahaba wa Mtume(Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) walirtadi (walitoka katika dini ya Kiislam) mara
baada ya kufariki Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa
Ahli Bayti na watu wachache wengine kama vile Suleiman na Ammar na Bilal
Radhiya Llahu Taala anhum.
Ama kuhusu Masahaba wawili wakubwa, nao ni Abubakar na ''Umar Radhiya Llahu Taala anhuma, ndani ya
vitabu vyao mna maelezo mengi sana yasiyohesabika katika kuwakufurisha.
Miongni mwa maelezo hayo ni
kauli zilizoandikwa katika kitabu cha Al Kiliniy - ukurasa wa ishirini, pale
aliposema;
"Nilimuuliza Aba Jaafar juu ya Masahaba
wawili wakubwa hawa, akanambia;
'Wamefariki dunia bila ya kutubu wala kukumbuka
yale waliyomtendea Amiri wa Waislam (Ali bin Abi Talib(Radhiya
Allaahu 'anhu)), iwapate laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika wake na ya watu
wote kwa ujumla !!!!!."
Na ameandika pia katika ukurasa wa 107 kuwa;
"Unaniuliza juu ya Abubakar na ''Umar? Naapa kwa umri wangu
kuwa wamefanya unafiki na kuyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu na kumfanyia mzaha
Mtume Wake na hawa ndio makafiri wawili, iwapate laana ya Mwenyezi Mungu na ya
Malaika na ya watu wote kwa ujumla!!!!!!!!!!"
Baada ya yote haya, ewe
mwenye kufuata madhehebu ya Kishia, kweli inaingia akilini kuwahukumu kuwa
makafiri na kuwa wamertaddi Masahaba wa Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) ambao ni wanafunzi wake na wao ndio walioinusuru dini yake na
waloibeba sharia yake, hawa ambao Mwenyezi Mungu ametaja kuridhika Kwake nao
katika kitabu chake na kuwabashiria Pepo kwa ulimi wa Mtume wake(Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam).
Mwenyezi Mungu amewachagua hawa kuwa walinzi wa dini Yake na kuitukuza dini Yake na kuwafanya waendelee
kutajwa ndani ya Qur-aan mpaka Siku ya Kiama. Hebu kwa ajili ya Mola wako sema
ewe mwenye kufuata Madhehebu ya Kishia; Katika kuwakufurisha na kuwalani na
kuwatoa katika Uislam Masahaba hawa wa Mtume(Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) si pana lengo lililokusudiwa?
Bila shaka yoyote ewe mwenye kufuata Madhehebu
ya Kishia, lengo lake ni kuupiga vita Uislam ambao ni
adui mkubwa wa Mayahudi na Wamajusi na adui wa kila Shirki na kila mwenye
kumuabudu mwengine asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Kusudi la kuwakufurisha Masahaba wa Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni
kuirudisha dola ya ki Majusi iliyokuwa ikiongozwa na Kisra baada ya Uislam
kuzibomoa nguzo zake na kuziangusha arshi zake na kufuta kuwepo kwake na hayo
yataendelea milele Inshaallah Taala.
Hebu tizama
mwenyewe dalili zisizohitaji kushereheshwa.
Aliyemuuwa Khalifa wa
pili wa Kiislam ni nani mwingine kama si kijana wa Ki Majusi?
Aliyeibeba bendera ya fitna dhidi ya 'Uthmaan(Radhiya Allaahu 'anhu) na kusababisha kuuliwa na
hapo ndipo mbegu ya mwanzo ya shari na fitna ilipopandishwa katika ardhi ya
Waislam ni nani mwingine isipokuwa Myahudi Abdillahi bin Saba-a?
Kutokana na mimba ovu hii akazaliwa Shetani wa
Kishia akiwa amebeba bendera ya Uzushi iitwayo (Wilaya ya Imam), na kuwa mfano
wa panga mbili zilizoelekezewa juu ya kichwa cha Uislam na Waislam katika
kuwaita watu katika utawala wa Maimam na kuwakufurisha Masahaba wa Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kuwalani
na kumkufurisha kila aliyeridhika nao au kuwataka watu waridhike nao katika
Waislam.
Kutokana na Uzushi wa Uimam zikapangwa hila
nyingi dhidi ya Makhalifa wa Kiislam na vita vingi vikali kuchochewa na damu
kumwagika na misingi kubomoka na Uislam ukaishi katika mfarakano, maadui walio
ndani yake ni sawa na maadui walio nje yake na wapinzani wake wanaojinasibisha
nao wakiwa sawa na maadui zake walioukanusha.
Kutokana na yote
haya, ewe mwenye kufuata Madhehebu ya Kishia, ndio itikadi za Kishia zikawekwa
ili iwe dini nyingine mbali na dini ya Kiislam. Dini yenye asili
zake, chimbuko lake, vitabu vyake na
mafundisho yake, elimu na maarifa yake.
Katika risala hii niliutanguliza ushahidi juu
ya ukweli wa maneno haya, kwa hivyo rudia tena kuusoma
na utafakari vizuri iwapo bado unashaka yoyote ile.
Ingelikuwa kusudi lao
si baya, wasingeligeuza itikadi ya Wilaya kuwa ni jambo la kuwafarikisha
Waislam na kupandisha mbegu ya shari, fitina na uadui baina yao.
Miongoni mwa Ahli Ssunnah wal Jamaa-a ambao wao
ndio wanaostahiki kuitwa Waislam wa kweli hakuna hata
mmoja kati yao anayewachukia Ahlu l Bayt. Kwa nini basi kundi la Mashia peke
yao ndio wanaojipa haki ya kuwa wao ni wapenzi wa Ahli l Bayti na kuigeuza haki
hiyo kuwa ni lengo lao kubwa na kwa ajili hiyo kuwafanyia uadui Waislam, bali
wanawakufurisha na kuwalani kama tulivyoona katika ushahidi nilioutanguliza.
Na kuhusu Uimam pia; Si itakuwa upuuzi na
ujinga iwapo Waislam hawatoachwa kujichagulia wenyewe mtu mahiri, mwenye sifa
za uongozi, wanayemuona kuwa anastahiki kuwaongoza na kuwahukumu kwa sheria ya
Mwenyezi Mungu na uongofu wa Mtume wake(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) kutokana na uwezo wake na uhodari wake?
Madhehebu ya Kishia yanasema;
"La - lazima awe aliyeusiwa kwa kutajwa na
awe amekingwa kutokana na madhambi na awe anafunuliwa Wahyi".
Lini Waislam watampata kiongozi wa aina hii? Kwa ajili hii ndiyo Mashia wanajitenga na kuwalani Waislam na kuwafanyia uadui?
Unaonaje ukaikomboa nafsi yako na usiwe mateka wa itikadi batili na kujitowa nje ya
madhehebu haya yasiyokuwa na nuru na yenye kuangamiza!!!?
Ewe mwenye kufuata Madhehebu ya Kishia; Kumbuka
kuwa utakuja kuulizwa juu ya nafsi yako na juu ya aila
yako. Kwa hivyo anza kuiokowa kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na juwa ya
kwamba hayo hayawi ila kwa kufuata Imani iliyo sahihi, na kwa matendo mema
yasiyopatikana isipokuwa katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na katika mafundisho
ya Mtume wake(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam). Na kumbuka pia kuwa wewe ukiwa ni mfungwa katika jela ya Madhehebu
mapotofu ya Kishia huwezi kuipata Imani iliyo sahihi wala kutenda matendo mema
ila iwapo utajiunga na Ahli Ssunnah wal Jamaa-a, hapo utakipata kitabu cha
Mwenyezi Mungu kilichotakasika na kisichochanganyika na taawil zisizokuwa
sahihi zilizoingizwa kusudi na viongozi wa Kishia kwa ajili ya kuwapotosha watu
na kwa ajili ya ufisadi.
Utayakuta pia Mafundisho ya Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyo sahihi yasiyochanganywa na uongo na upendeleo. Kwa ajili hiyo unaweza kuipata Imani
iliyo sahihi na Itikadi ya Kiislam iliyosalimika na
matendo mema yaliyowekewa sheria ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake ili
wajitakase kwayo nafsi zao, na yenye kuwapa ahadi ya ushindi.
Kwa hivyo ihame itikadi hiyo, ewe Mwenye
kufuata Itikadi ya Kishia na uelekee kwa Mola wako na Mafundisho ya Mtume wake(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani utapata
pahala pengi pa kukimbilia.
Mwisho kabisa, nataka uelewe kuwa mimi
sikukutangulizia NASAHA HII kwa ajili ya tamaa ya kile ulicho nacho au
kilichopo kwa binadamu yeyote yule mwengine, au kwa kukuogopa wewe au mwengine
yeyote yule katika wanadamu, sivyo Wallahi, bali nimekutangulizia haya kwa
ajili ya undugu katika Uislam na kwa ajili ya kuwajibika kupeana nasaha kwa
ajili ya kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya Kitabu chake na
Mafundisho ya Mtume wake(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kwa
ajili ya Waislam wote.
Haya ndiyo yaliyonifanya nikuletee Nasaha hii
nikitarajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu nasaha hii
ikufungue kifua chako na akuongoze katika yale yatakayokufurahisha katika dunia
yako na akhera yako.
Wasalaamun ala l Mursaliyna wal Hamdu li Llahi Rabi l
aalamiyn