UPOLE WA MUANU BIN ZAYEDA
Amiri huyu aliyekuwa akitawala nchi ya iraq alijulikana sana kwa ukarimu na upole wake, hata waarabu humpigia mfano, kwa kusema ; "Fulani mpole kuliko Muanu bin zayeda".
Mbedui mmoja aliposikia juu ya upole na ustahamilivu wa amiri huyu akaona bora ende kumjaribu.
Mbedui;
Kumbuka ewe wetu kiongozi unakumbuka ulipokuwa ukivaa ngozi na nguo za kifakiri?
Amiri Moanu bin Zayeda:
Nakumbuka hayo wala sisahau.
Mbedui:
Kwa hivyo mtukuze mola wako aliyekupa mawili - Kutawala nchi yako na kukuwezesha kuvaa na kukalia hariri.
Amiri Moanu bin Zayeda:
Subhaana llah, subhaana llah.
Mbedui:
Basi sikiliza mimi sitokupa heshima ya ki amiri, tena maneno haya naya nakariri maana hustahiki wewe salamu ya ki amiri.
Aamiri Moanu bin Zayeda:
Ewe Ndugu mwarabu! salamu ni sunnah, ukitaka toa, usipotaka usitoe.
Mbedui:
Kuishi katika nchi yako sitaki, bora niishi fakiri, nitaihama Iraqi madamu wewe amiri.
Amiri Moanu bin Zayeda:
Ewe ndugu wa kiarabu, kama unataka kuishi jirani na sisi, tunakukaribisha, la hutaki, tunakutakia usalama katika safari yako .
(kwa vile jina la babake amiri huyo ni Zayeda, na maana yake ni "aliyezidi", basi mbedui akambadilisha na kumwita "aliyepungua" .
Mbedui akasema:
Mwana wa alopungua, ninyoshee dinari mbili, safari nishaamua kesho mimi narahili
Aamiri Moanu bin Zayeda :
Mpeni dinari elfu zimsaidie katika safari yake.
Mbedui baada ya kuzipokea dinari elfu hizo akasema;
Kumbe wewe si mpaji kumbe wewe ni bakhili nilikuwa nataraji utanipa kwa kithiri
Amiri Moanu bin Zayeda:
Muongezeeni elfu nyingine.
Mbedui alizipokea kisha akasema;
Namuomba mtukufu, akupe nguvu tamamu sijaona wako kufu baina ya wanadamu.
Aamiri Moanu bin Zayeda:
Muongezeeni elfu nyingine.
Mbedui (baada ya kuzipokea);
Ewe amiri, mimi nimekuja na nia ya kukujaribu upole wako kutokana na niliyokuwa nikiyasikia juu yako. kwa hakika Mwenyezi Mungu amekupa upole ambao wangeligawiwa watu wote duniani basi ungewatosha .
Amiri Moanu bin Zayeda:
Ewe kijana, dinari ngapi ulizokwishampa?
Kijana:
Dinari elfu tatu.
Amiri Moanu bin Zayeda:
Muongezee dinari elfu tatu nyingine .
Mbedui alizichukua dinari hizo na kumshukuru kwa ukarimu wake.
Kwa ajili hii akawa anapigiwa mifano amiri huyo kwa upole na ukarimu wake.
MUHAMMAD FARAJ SALEM AL SAIY