Mafunzo Kutoka Katika Hijrah
Muhammad Faraj Salem Al Saiy
Ndugu
zangu Waislam, kalenda ya Hijri (Kalenda ya Kiislam) imeanza, na kwa ajili hiyo tutajikumbusha kidogo juu ya umuhimu wa
siku hizi kwa ajili ya kuelewa umuhimu wake na kwa ajili ya kujifunza angalau
machache juu ya Hijrah ya Mtume wetu mtukufu Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) pamoja na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhu).
Mwaka
jana katika mnasaba huu, tulisoma namna gani tukio la Hijrah lilivyokuwa muhimu
kupita matukio yote yaliyopata kutokea katika historia ya Kiislam, na hii ni
kwa sababu kutokana na Hijrah, taifa la mwanzo la Kiislam liliweza kuundwa, na
Waislamu wakaweza kuweka miguu yao juu ya ardhi, madhubuti kwa ajili ya
kuisimamisha dini yao, kuilinda itikadi yako, na kuweza kuieneza ulimwenguni
kote.
Mtume
Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na Waislamu wa mwanzo
waliokuwa wachache sana, wakiongozwa na Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan na ‘Aliy
(Radhiya Llaahu ‘anhum), walihiari kuhatarisha maisha yao, kupoteza mali zao,
milki zao pamoja na kila walichokuwa nacho kwa ajili ya kutaka radhi za Mola
wao Subhaanahu wa Ta’ala.
Allaah
Anasema:
{{Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na walio pamoja
naye wana nguvu mbele ya makafiri, na wanahurumiana
wao kwa wao. Utawaona wakiinama na kusujudu wakitafuta
fadhila na radhi za Allaah.}} [Al-Fath:
29]
Tukasema
kuwa kwa ajili ya umuhimu wake, ndiyo maana Waislam
walikubaliana kuianzisha Kalenda ya Hijrah ya Kiislam kuanzia mwaka huo.
Siku
tukufu ambayo Mtume wetu Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akifuatana na Sahibu yake Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu),
walihama kutoka Makkah kwenda Madiynah, wakitanguliwa na kufuatiliwa na Maswahaba
watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum).
Waislamu
ambao wakati huo walikuwa wachache sana, walipata
mtihani mkubwa kutokana na mateso waliyopata pamoja na kudharauliwa na
kunyanyaswa na makafiri wa Makkah. Lakini mara baada ya kutakiwa na Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuihama nchi
yao hiyo na kwenda Madiynah, wakaanza kukumbana na mtihani mwingine. Mtihani wa kuiacha nchi yao, nchi waliyozaliwa na kulelewa na
kucheza juu ya mchanga wake. Iliwabidi waiache nchi hiyo pamoja na kuacha nyuma mali zao, nyumba zao na kila walichomiliki
isipokuwa vichache sana walivyoweza kuvibeba katika safari ndefu iliyojaa kila
aina ya hatari na mashaka. Walikuwa tayari kupambana na
yote hayo kwa ajili ya utiifu wao kwa Mola wao na kwa ajili ya kuinusuru na
kuiendeleza dini yao.
Kwa
vile wengi wao walitoka nyakati za usiku kwa kujificha wakihofia maisha yao,
iliwabidi waache vitu vyao vingi vilivyokuwa vizito na vengine vya thamani, ili
waweze kukimbia kwa wepesi na haraka na ili wasalimike na mateso ya Maquraysh.
Waliacha vyote hivyo nyuma yao na kuianza safari ndefu iliyowawezesha kufika
kwa ndugu zao waliokuwa wakiwasubiri kwa hamu na shauku kubwa sana huko Madiynah
ili washirikiane nao katika kuiendeleza mbele dini yao hii tukufu na mpya.
Anasema Ibn Kathiyr katika Al-Bidaayah wan Nihaayah kuwa:
"Katika
mwaka wa kumi na sita na inasemekana katika mwaka wa kumi na saba wa Ukhalifa
wa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu), Waislam walikubaliana
kuianzisha Kalenda yao, kutokana na matatizo yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara
baina yao wakati watu wakiandikiana mikataba ya madeni au ya aina nyengine.
Waarabu
walikuwa wanayohesabu ya miezi yao, lakini hawakuwa na
hesabu ya miaka, na kwa ajili hiyo wengine walikuwa wakitumia kalenda za
Kifursi na wengine za Kirumi na wengine wakitumia matukio ya wakati wa
ujahilia.
‘Umar
(Radhiya Llaahu ‘anhu) alipowataka Waislam kutoa rai zao kuhusu jambo hilo,
wengine wakapendekeza ianzie mwaka aliozaliwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam) na wengine wakapendekeza ianzie pale alipopewa Utume na wengine
wakapendekeza siku aliyokufa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Lakini
Khalifa wa Waislam ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya
Llaahu ‘anhu) akapendelea rai zilizosema kuwa ianzie siku ile ya Hijrah na
wengi wakakubaliana naye.
Kwa
vile mwezi wa Muharram ndio mwezi wa mwanzo wa Kiarabu,
wakakubaliana kuhesabu kuanzia mwezi huo."
Ufuatao
ni mpangilio wa Miezi ya Kiislam:
MUHARRAM (Mfunguo nne)
Swafar
Rabiy’ul Awwal (Mfunguo sita)
Rabiy’uth Thaaniy
Jumaadal Awwal
Jumaadath Thaaniy
RAJAB
Sha’abaan
Ramadhaan
Shawwaal
DHUL QA’DAH (Mfunguo pili)
DHUL HIJJAH (Mfunguo tatu)
Baada
ya kutoa dalili mbali mbali, Mwanachuoni Ibn Kathiyr katika kitabu chake hicho
mashuhuri kiitwacho Al-Bidaayah wan Nihaayah
akamaliza kwa kusema:
"Nimekuelezeeni
kwa ushahidi wa kutosha ulioandamana na isnadi zake na njia zake kutoka katika
Siyrah ya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) na AlhamduliLlaah na
kusudi langu ni kuwa wao (Maswahaba) walikubaliana wote kwa Ijmai kuianzisha
Kalenda ya Kiislam kuanzia Mwaka wa Hijrah na wakakubaliana kuufanya mwezi wa
mwanzo uwe mwezi wa Muharram na hii pia ni kauli za Maimaam wote
waliobaki".
Ama
kuhusu rai ya Imaam Maalik, Ibn Kathiyr ameandika yafuatayo:
"Amesema
As-Suhayliy na wengineo kuwa Imaam Malik amesema
kwamba mwanzo wa Mwaka wa Kiislam ungeanzia mwezi wa Rabiy’ul-Awwal (na si
Muharram), kwa sababu mwezi huo ndio aliohama ndani yake Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam), na akaegemea ushahidi wake katika kauli ya Allaah Subhanahu
wa Ta’ala pale Aliposema:
{{Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa kumcha Allaah
tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame humo.}} [At-Tawbah: 108]
(Kusudi
la 'Siku ya mwanzo' katika Aayah hii, ni siku ile
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipowasili Madiynah).
"Bila
shaka kauli ya Imaam Malik ndio inayonasibiana, lakini (Maswahaba kabla yake)
walikwishakubaliana kuwa Mwaka wa Kiislam uanzie Mwaka
aliohama Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ndani yake (Mwaka wa Al-Hijrah),
na wakakubaliana Mwezi wa mwanzo uwe mwezi wa Muharram ili wasibabaike. Wa-Allaahu Ta’ala A’alam”.
Hivi ndivyo alivyomaliza Imaam Al-Haafidh Ibn Kathiyr
(Rahimahu Allaah).
Safari
za jangwani zilikuwa zikiwatoa jasho majabari na mashujaa wakubwa wa wakati ule
wanaosafiri wakiwa katika amani, kwa hivyo munaweza kukisia hatari za namna
gani zilizokuwa zikimkabili Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
aliyeondoka akiwa na sahibu yake Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu) huku
wakiwa wanasakwa na makafiri waliokwishaamua kuwa lazima auliwe, wakatangaza
zawadi ya ngamia mia moja kwa yeyote atakayeweza kumkamata Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) akiwa hai au amekwishakufa.
Hawezi
kuyakisia haya ila yule aliyewahi kuuonja moto wake.
Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kulikata jangwa lile alipokuwa mdogo
akiwa amefuatana na mama yake siku ile walipokwenda
Madiynah kwa ajili ya kulizuru kaburi la baba yake, kisha akarudi Makkah peke
yake kwa sababu mama yake alifariki dunia alipowasili Madiynah. Lakini safari
hii Muhammad (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) analikata tena jangwa hilo hilo akiwa na umri uliopindukia miaka hamsini pamoja na
Sahibu yake Asw-Swiddiyq (Radhiya Llaahu ‘anhu), si kwa ajili ya matembezi wala
kwa ajili ya biashara, bali kwa ajili ya kuuendeleza ujumbe aliokuja nao.
Anasafiri
ili aweze kuusimamisha ujumbe huo juu ya ardhi ya
Yathrib (Madiynah), na kuiweka mizizi yake hapo baada ya kung'olewa katika mji
wa Makkah.
Aliondoka
Makkah kuelekea Madiynah akiwa na yakini kupita mtu
yeyote yule kuwa Mola wake Atamnusuru na kuidhihirisha dini Yake, na alikuwa na
uhakika pia kuwa Mola wake atamrudisha tena Makkah.
Allaah
Alikwishamwambia:
{{Na hakika wewe uko mbele ya macho Yetu.}} [Atw-Twuur: 48]
Na Akasema:
{{Hakika Yeye Aliyekulazimisha (kufuata) Qur-aan, kwa
yakini Atakurudisha mahali pa kurejea.}} [Al-Qaswasw: 85]
Mwenendo Wa
Mitume ('Alayhimus Salaam)
Kutokana
na Hijrah hii Mtume wetu mtukufu (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) atakuwa ametimiza Sunnah ya Mitume wenzake waliomtangulia,
kwani Mitume yote ('Alayhimus Salaam) kuanzia Nabii Ibraahiym mpaka kufikia kwa
‘Iysa (‘Alayhis Salaam), wote waliihama miji yao waliyozaliwa, wakateswa na
kusubiri ili wawe mfano mwema kwa watu wao.
Na
hii ndiyo maana Waraqah bin Nawfal siku ile alimwambia Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam):
"Yareti ningeliishi mpaka siku ile watu wako
watakapokutowa katika nchi yako".
Na Allaah
Amesema:
{{Na wale waliokufuru wakawaambia Mitume yao:
"Tutakutoeni katika nchi yetu au lazima murudi katika mila yetu.}} [Ibraahiym: 13]
Tofauti Ya Kuhama Kwa Mtume
(Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Na Kuhama Kwa ‘Umar Bin Al-Khattwaab (Radhiya
Llaahu ‘Anhu)
"Inaweza
kumpitikia mtu kutaka kufananisha baina ya kuhama kwa
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kuhama kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab
(Radhiya Llaahu ‘anhu), akajiuliza:
"Kwa
nini ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) akahama mchana tena mbele ya watu bila
kuogopa, huku akiwabishia makafiri pale alipowaendea na
kuwaambia:
‘Zimedhalilika
nyuso zenu, zimedhalilika nyuso zenu, yeyote kati yenu anayetaka mamake
ampoteze na wanawe wawe mayatima na mkewe awe kizuka,
basi na akutane nami nyuma ya bonde hili.’
Wakati
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alihama kwa
kificho bila kumjuulisha mtu. Mtu anaweza kujiuliza:
"Hivyo ‘Umar (Radhiya Llaahu ‘anhu) anaweza
kuwa shujaa kuliko Mtume?
Jibu lake litakuwa:
"Umar
bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) au Muislam yeyote yule, hukmu yao ni
tofauti na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), kwani matendo ya mtu yeyote
yule awe ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu) au mwengine yanahesabiwa
katika dini kuwa ni matendo yake mwenyewe binafsi, na kwamba si hoja inayoweza
kusimama katika dini kama yalivyo matendo ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa
sallam). Kwani mtu mwingine asiyekuwa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
anaweza kutumia njia zozote zile azitakazo anazoziona kuwa ni mnasaba kwake,
ama Mtume wa Allaah (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) yeye matendo yake ni Shari’ah,
na hii maana yake ni kuwa matendo yake yote yanayohusiana na dini yanahesabiwa
kuwa ni Shari’ah kwetu, na kwa ajili hiyo Mafundisho yake (Sunnah zake) yakawa
ni asili ya pili ya Shari’ah, yakiwemo matendo yake, maneno yake, sifa zake na
yale yaliyofanywa mbele yake na akayakubali.
Lau kama Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) angefanya kama
alivyofanya ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Llaahu ‘anhu), baadhi ya watu
wangedhania kuwa hivyo ndivyo anavyowajibikiwa kila Muislam kufanya, na kwamba
haina haja mtu kuchukua tahadhari wala kuogopa pale anapokuwa katika hatari.
Baada Ya Kuhamia Madiynah
Tuliona
huko nyuma kuwa mara baada ya kuwasili mjini Madiynah, jambo la mwanzo alilofanya
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) ni kufungisha udugu baina ya watu wa
Makkah na watu wa Madiynah, na jambo la pili ni kuujenga Msikiti uliokuwa mfano
wa Chuo Kikuu kilichokuwa kikifundisha Imani, udugu, umoja, ushujaa, fiqhi
pamoja na tabia na mwenendo mwema, na kutokana na hayo Chuo hicho kikaweza
kutoa mashujaa walioweza kuzifungua nchi nyingi pamoja na nyoyo nyingi.
Mtume (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Akiwa Madiynah
Anasema
Shaykh Abu Bakr Al-Jazairiy:
"Hakika
ya miaka yote kumi na tatu aliloishi Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
pale Makkah tokea alipopewa utume mpaka siku ile aliyohama kwenda Madiynah,
yote ilikuwa ni maumivu na machozi na huzuni. Hakupata kufurahi hata kwa muda wa saa moja au kustarehe angalau kwa siku moja.
Ama
miaka kumi aliloishi Madiynah, yote ilikuwa ni miaka
ya Jihaad iliyokamatana. Hakupata hata siku moja kukaa bure
wala kustarehe. Hata maisha; kwake yalikuwa magumu,
hakupata hata siku moja kushiba mkate au tende wala hata kula vizuri mara mbili
katika siku moja.
Naam, ingawaje kwa siku alizoishi Madiynah zilikuwa
ni siku za kuchomoza, lakini siku nyingi katika hizo zilikuwa ni za
kuunguza".
Kusilimu Kwa ‘Abdullaah Bin
Salaam (Radhiya Llaahu ‘Anhu)
Mara
baada ya Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kuwasili mji wa Madiynah alikuja kwake ‘Abdullaah bin Salaam (Radhiya
Llaahu ‘anhu) na kuzitamka shahada mbili.
Akasema:
"Nashuhudia kuwa hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba wewe ni Mtume wa Allaah na kwamba uliyokuja nayo
ni haki. Ee Mtume wa Allaah, Mayahudi ni watu waongo, wanajua kuwa mimi ni
bwana wao na mwana wa bwana wao na wanajuwa pia kuwa mimi ni ‘Aalim wao na
mwana wa ‘Aalim wao, kwa hivyo nakuomba (uniache nijifiche, kisha) uwaite na uwaulize
juu yangu kabla ya kuwajulisha juu ya kusilimu kwangu, kwani wakijua kuwa
nimesilimu watasema juu yangu yale nisiyokuwa nayo".
Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaita Mayahudi, na
walipohudhuria akawaambia:
((Enyi
Mayahudi! Adhabu kali itakufikieni, mcheni Allaah, Naapa kwa
yule ambaye hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Yeye, kuwa munajua vizuri
kwamba mimi ni Mtume wa kweli wa Allaah na kwamba niliyokuja nayo ni haki, kwa hivyo
ingieni katika dini ya Kiislam.))
Wakasema
mara tatu:
"Sisi
hatujui"
Kisha
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:
((Ana
daraja gani kwenu ‘Abdullaah bin Salaam?))
Wakasema:
"Yule ni bwana wetu na mwana wa bwana wetu, na ‘Aalim kutupita sote
na mwana wa ‘aalim kutupita sote".
Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:
((Munaonaje akisilimu?))
Wakasema:
"Haiwezekani
hata siku moja akasilimu"
Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza hivyo mara tatu, kisha akasema:
((Ee
‘Abdullaah bin Salaam, watokee.))
Akawatokea
na kusema:
"Enyi Mayahudi, mcheni Allaah kwani naapa kwa
yule ambaye hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Yeye, mnajua vizuri kuwa huyu
ni Mtume wa Allaah na kwamba amekuja na haki".
Wakasema:
"Muongo! wewe si bwana wetu wala si ‘Aalim wetu".
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaamrisha watolewe nje.
[Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Mwenye Kumtii Mtume (Swalla
Llaahu ‘Alayhi Wa Sallam) Atakuwa Pamoja Naye
Maswahaba wa Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na hususan watu
wa Madiynah walikuwa
wakimpenda Mtume wao (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) kupita kiasi, na
walikuwa tayari wakati wote kuzitanguliza roho zao na nafsi zao kwa ajili ya
kumlinda Mtume wao mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na yale
aliyokuja nayo. Ni wao waliohatarisha maisha yao hapo
mwanzo walipomfuata Mtume wao mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) huko
Makkah katika usiku ule wa hatari na kumpa ahadi ya kumnusuru na kumlinda ikiwa
atahamia kwao Madiynah. Kisha wakafungamana naye kwa siri mahali panapoitwa Al-’Aqabah
katika mafungamano yaliyokokuja kujulikana baadaye kama
'Fungamano la ‘Aqabah' (la mwanzo na la pili).
Watu wa Madiynah waliitimiza ahadi yao hiyo ya kumlinda Mtume wao
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na kuwalinda Waislam wote waliohamia
kwao na kuwasaidia kwa hali na mali. Na pale Allaah Subhaanahu Wa Ta’ala Alipoiteremsha kauli Yake:
{{Wameruhusiwa
(kupigana vita) wale wanaopigwa kwa sababu
wamedhulumiwa. Na kwa yakini Allaah ni Muweza wa
kuwasaidia. Ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki ila
kwa sababu wanasema; "Mola wetu ni Allaah.}} [Al-Hajj: 39-40]
Watu wa Madiynah wakaingia katika mapambano mbali mbali na
majeshi ya makafiri mpaka pale Allaah alipowawezesha Waislamu kuuteka mji wa
Makkah na kuyabomoa masanamu yaliyokuwepo ndani ya Al-Ka’abah na kuidhihirisha
Haki na kuiangamiza Baatwil.
Hadiyth
ifuatayo inatuwezesha kuihisi angalau kwa uhaba ladha ya namna Maswahaba
(Radhiya Llaahu ‘anhum) na hasa watu wa Madiynah walivyokuwa wakimpenda na
kumuenzi na kumthamini Mtume wao mtukufu (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na
namna gani walivyokuwa tayari kujitolea kwa hali na mali kumtii Mtume wa Allaah
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Imetolewa
na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim na Atw-Twabaraaniy na
wengineo kuwa mara baada ya kumalizika vita vya kuuteka mji wa Makkah, Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) aliwakusanya mateka na kuwauliza:
((Mnadhani nitakufanyeni nini?))
Wakajibu:
((Utatufanyia
kila la kheri, ewe ndugu mwema na mwana wa ndugu
mwema.))
Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:
((Nendeni, nyote nimekuacheni huru.))
Karibu
mateka wote hao wakasilimu kwa hiari yao na kujiunga
na jeshi la Kiislamu lililoondoka hapo Makkah kuelekea mji wa Hunayn kwa ajili
ya kupambana na majeshi ya watu wa Huwzan waliokuwa njiani kuelekea Makkah
kuwashambulia Waislam.
Imepokelewa
kutoka kwa ‘Abdullaah bin Zayd (Radhiya Llaahu ‘anhu)
kuwa baada ya Waislam kushinda katika vita vya Hunayn, Mtume (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) aliwagawia ngawira iliyopatikana katika vita hivyo watu wa
Makkah tu hasa wale waliosilimu hivi karibuni kwa ajili ya kuwalainisha nyoyo
zao, na watu wa Madiynah hawakupewa chochote.
Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) alijuwa kuwa watu wa Madiynah
hawakufurahi kwa sababu na wao pia walitegemea kupewa chochote katika ngawira
ile kama walivyopewa wenzao watu wa Makkah.
Alipojulishwa
juu ya hayo, Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaita watu wa Madiynah na kuwahutubia, akasema:
((Nini haya maneno niliyosikia kuwa mlikuwa
mkiyasema?))
Viongozi
wao wakasema:
"Ama wakubwa wetu hawakusema lolote, isipokuwa watu wengine
wanasema; "Allaah Amghufirie Mtume wake, anawapa Maquraysh ngawira kwa mamia na sisi hatupi chochote wakati damu zao bado hata
hazijakauka juu ya panga zetu?"
Mtume (Swalla
Llaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
((Mmekasirika
kwa sababu ya faida ndogo tu ya kidunia enyi watu wa
Madiynah? Mimi nimewapa hawa kwa sababu wao ndio
kwanza wametoka katika ukafiri na kuingia katika Uislam ili niwalainishe nyoyo
zao, nikakuacheni nyinyi kwa kuutegemea Uislam wenu. Enyi watu wa Madiynah! Si niliwakuta mmepotoka Allaah
Akakuongozeni kupitia kwangu? Na nikawakuta masikini na
Allaah Akakutajirisheni kupitia kwangu? Mmegawanyika na
Allaah Akakuunganisheni kupitia kwangu? Mafakiri na Allaah
Akakuneemesheni kupitia kwangu?))
Walikuwa
kila wanapoulizwa wakijibu:
"Allaah Ametufanyia ihsani zaidi na Mtume
Wake ametufanyia Ihsani zaidi"
Mtume
(Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawauliza:
((Mbona hamnijibu?))
Wakasema:
"Tukujibu nini ee Mtume wa Allaah?"
Akasema:
((Kama
mngenijibu kwa maneno mengine zaidi ya haya mngekuwa
mnasema kweli. Mngetaka, mngeweza kusema; "Na wewe pia
ulikuja kwetu ukiwa umefukuzwa na watu wako na sisi tukakupokea, umekadhibishwa
na sisi tukakusadiki. Ulikuja peke yako umo hatarini na
sisi tukakunusuru, na tukayakubali yale watu wako waliyoyakataa. Kisha mkawa mnanihesabia mema yote mliyonitendea.))
Kisha
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akawaambia:
((Hamridhiki
wakati wenzenu wanaondoka wakiwa na ngamia na kondoo
na nyinyi mtaondoka mkiwa na Mtume wa Allaah mpaka makwenu? Watu wa Madiynah (Al-Answaar) ni mfano wa nguo iliyokamatana na
ngozi na waliobaki ni mfano wa guo la juu, Enyi watu wa Madiynah! Si Allaah Amekuiteni
majina mazuri mazuri (kama vile) 'Answaar wa Allaah'
na 'Answaar wa Mtume Wake?' Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake,
lau kama nisingehajiri basi ningelikuwa mmoja kati ya watu wa Madiynah, na lau
kama watu wote watafuata njia zao katika mabonde na mitaa, na watu wa Madiynah
watafuata njia nyingine, basi mimi ningefuata njia ya watu Madiynah. Allaah Warehemu
ma-Answaar (watu wa Madiynah) na wana wa Answaar na
wajukuu wa Answaar.))
Anasema
Ibn Is-haaq aliyoisimulia sehemu ya mwisho ya Hadiyth hii kuwa:
"Waliohudhuria
wakaanza kulia kwa kwikwi mpaka ndevu zao zikarowa, wakasema:
"Tumeridhika na Allaah kuwa Mola wetu na
Mtume Wake kuwa sehemu yetu."
Kisha
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) akaondoka na
wao wakatawanyika.
Sehemu ya
mwisho ya Hadiyth hii imepokelewa kwa njia ya Imaam
Ahmad peke yake na kusimuliwa na Ibn Is-haaq.
Ndugu
zangu Waislam, anayetaka kuwa pamoja na Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam)
na Maswahaba wake watukufu (Radhiya Llaahu ‘anhum) siku ya Qiyaamah, lazima awe
mtiifu wa maamrisho aliyokuja nayo Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam).
Imepokelewa
na Atw-Twabaraaniy na Ibn Mardawiya na Abu Na’iym kutoka
kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah bint Abi Bakr (Radhiya Llahu anhum) kuwa: Siku
moja mtu mmoja alimwendea Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:
"Ee Mtume wa Allaah, kwa hakika mimi
nakupenda kuliko ninavyoipenda nafsi yangu na kuliko ninavyowapenda wanangu. Ninapokuwa nyumbani basi nikikukumbuka tu, siwezi kustahamili tena,
lazima nije nikutazame. Lakini kila ninapokumbuka kuwa siku moja mimi nitakufa na wewe utakufa, kisha nikakumbuka kwamba wewe
daraja yako itakuwa juu pamoja na Mitume, na mimi nikiingia Peponi naogopa
(daraja yangu haitokuwa ya juu kama yako) nisiweze kukuona tena huko".
Katika
riwaya nyingine:
"Swahaba
yule aliyekuwa katika watu wa Madiynah alilia sana, na
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) alipomuuliza:
((Nini kinachokuliza?))
Akamjibu:
"Kila ninapokumbuka kuwa wewe daraja yako itakuwa ya juu pamoja na Mitume, na mimi nikiingia Peponi naogopa (daraja yangu
haitokuwa ya juu kama yako) na sitoweza kukuona tena huko".
Kabla
Mtume (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwahi kumjibu Swahaba yule (Radhiya
Llaahu ‘anhu), Jibriyl (‘Alayhis Salaam) aliteremka na
kauli ya Allaah isemayo:
{{Na Mwenye kumtii Allaah na
Mtume, basi hao watakuwa pamoja na wale Aliowaneemesha Allaah; Manabii na Swddiqiyn
na Mashahidi na Swaalihiyn (watu wema). Na uzuri ulioje (kwa
mtu) watu hao kuwa rafiki (zake).}} [An-Nisaa: 69]
Yaani
atakayefanya yale aliyoamrishwa na Mola wake na Mtume wake (Swalla Llaahu
‘alayhi wa sallam) na akayaacha yale alokatazwa na Mola wake na aliokatazwa na
Mtume wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam), basi Allaah Atamuingiza katika
Pepo yake na atakuwa pamoja na Manabii na Swiddiqiyn na Mashahidi na Swaalihiyn
(watu wema).