KUKUNJA MIKONO KATIKA SALA
Ndugu zangu Waislam
Assalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
Kukunja mikono si kitendo kilichotendwa
na Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) peke yake, bali alikuwa akisisitiza na
kuwasahihisha wale waliokuwa wakikunja mikono
Anasema Imam Malik (Mwenyezi Mungu amrehemu) katika kitabu cha Al Muwatta, na huyu ni Imam wa watu wa Madina mji alioishi na kusali
ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu zaidi ya miaka kumi, na Masahaba wake
watukufu (RA) wakaendelea kusali hapo miaka mingi iliyofuata.
Katika ukurasa wa 122 na 123 mlango wa "Mwenye kusali aweke mkono mmoja
juu ya mwengine", imeandikwa katika kitabu hicho cha Imam Malik
katika hadithi nambari 133 kama ifuatavyo;
"Katika maneno ya Mitume ni kuwa usipokuwa na haya basi fanya utakalo, na
pia (katika maneno ya Mitume) ni kuweka mkono mmoja juu ya mwengine katika Sala."
Haya ni maneno ya Imam Malik ndani ya kitabu chake cha
Al Muwatta.
Na katika kitabu hicho hicho cha Al Muwatta Imam Malik ameandika hadithi
kutoka kwa Sahl bin Saad Al Saaidiy kuwa; Watu
walikuwa wakiamrishwa kuweka mkono wao wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika
Sala."
Anasema Abu Hazim;
"Naelewa kuwa anakusudia hapa wakati wa Mtume wa
Mwenyezi Mungu (SAW)".
Bukhari Juz. 1 ukurasa wa 397 Imam Malik katika
Muwataa na Imam Ahmed katika
Musnad
Na katika kuisherehesha hadithi hiyo amesema Imam Malik (Mwenyezi Mungu
amrehemu);
"Kuweka (mkono) wa kulia juu ya kushoto
na kuharakisha futari na kuchelewesha daku."
Haya ameyasema katika kuisherehesha hadithi
iliyotangulia ya Abil Mukhariq.
Abil Mukhariq
Baadhi ya watu wakasema kuwa katika hadithi iliyomo ndani ya Muwatta
yumo Abil Mukhariq na huyu anajulikana kuwa ni dhaifu katika elimu ya hadithi,
lakini inaeleweka pia katika elimu ya hadithi kuwa udhaifu wa wapokeza
unakhitalifiana darja, na kwamba daraja inayokubalika hadithi zao katika
madhaifu ni wale waliodhoofishwa kwa ajili ya udhaifu wao wa kuhifadhi ikiwa
wao si watu waongo wala si wenye kupenda kuongeza maneno.
Madhaifu wa aina hii anasema Dr. Mohd Ajjaj al
Khatib katika kitabu chake cha 'Al Mkhtasar al wajiyz fiy Uluum al Hadiyth
kuwa;
"Mtu aliyedhoofishwa kwa ajili ya kuhifadhi kwake, au kwa ajili ya
kutoweza kudhibiti maneno vizuri, ikiwa hatuhumiwa kwa ila nyingine, na ikiwa
zitapokewa hadithi zake kwa njia nyingi, basi hadithi itapanda na kufikia darja
ya hadithi 'Hassan', na kwa ajili hiyo udhaifu wake unatoweka kwa kupokelewa
hadithi kwa njia nyingine."
Anasema Imam Muhammad bin Al Hassan Al Sheibaniy kuwa;
"Anatuhumiwa Abil Mukhariq kwa udhaifu
wake wa kuhifadhi tu."
Isitoshe ndani ya kitabu hicho cha Al Muwatta ipo pia hadithi iliyosimuliwa
na Ibni Abbas (RA) na kunukuliwa pia na Maimam Ahmed
na Bukhari na wengineo, inayosema;
"Watu (wakati wa Mtume (SAW)) walikuwa
wakiamrishwa kuweka mikono
Hapana hadithi sahihi hata moja kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi
Mungu (SAW) inayosema kuwa alikuwa akifanya kinyume cha hivyo, na hii ni kauli
ya wengi
Bidayatul Mujitahid
Yaliyoandikwa ndani ya kitabu cha Bidyatul Mujtahid si kukanusha kufunga
mikono bali ni kuthibitisha, isipokuwa tu imenukuliwa ndani ya kitabu hicho kuwa
Imam Malik amejuzisha kukunja katika sala ya Sunnah na hakujuzisha katika sala
ya Fardhi akihofia watu wasiwe wanafunga kwa ajili ya kujipumzisha tu na
wasidhani kuwa ni nguzo mojawapo ya Sala na kwamba Sala inabatilika iwapo mtu
atafanya kinyume cha hivyo. (hii ikiwa kweli
imethibiti kuwa Imam Malik amesema hayo), lakini yaliyomo ndani ya kitabu chake
cha Al Muwatta ni kinyume na hayo.
Hadithi za Kukunja Mikono
Ama hadithi zinazoeleza juu ya kukunja mikono ni
nyingi
Na katika Sunan za Abu Daud hadithi iliyosahihishwa na
Ibni Khuzaymah
inasema;
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya mkono
wa kushoto."
Na katika hadithi iliyopokelewa na Attabarani na Ibni
Habban, anasema
'Bahari ya elimu' Ibni Abbas (RA) kuwa;
"Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) amesema;
"Sisi Mitume tumeamrishwa kuharakisha kula futari zetu na kuchelewesha
kula
daku letu, na kuweka mikono yetu ya kulia juu ya kushoto ndani ya Sala."
Imepokelewa pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu
(SAW) alipomuona mtu mmoja akisali huku ameuweka mkono wake wa kushoto juu ya
mkono wa kulia, akauondoa na kuuweka wa kulia juu ya kushoto."
Ahmed na Abu Daud.
Na imepokelewa kutoka kwa Sahaba Abu Hurairah (RA)
kuwa katika Sala ya maiti Mtume wa Mweyezi Mungu alinyanyua mikono yake juu
akasema 'Allahu Akbar', kisha akauweka mkono wake wa kulia juu ya wa kushoto."
Attirmidhiy katika 'Baab maa jaa fiy rafail yadayni.
Imepokelewa katika Sahih Muslim na kutoka kwa
Imam Ahmed na Attabarani kuwa;
"Na alikuwa akiuweka mkono wake wa kulia juu ya sehemu ya nyuma ya mkono
wa kushoto."
Katika mlango huu zimepokelewa hadithi zaidi ya ishirini kutoka kwa Masahaba kumi
na nane pamoja na waliowafuatilia (Attabiina), zote hizo zikitoka moja kwa
moja kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW)
(Nanukuu kutoka katika kitabu cha 'Akhtaal Musalliyn' (makosa yanayofanywa
katika Sala) kilichoandikwa na Mashahur Hassan Suleiman) anasema:
Imepokelewa pia kutoka kwa Wail bin Hajar kuwa amesema;
"Kama kwamba namtizama Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW) namna alivyokuwa
akisali", akasema:
"Nikamtizama! akatoa takbir, kisha akanyanyua
mikono yake mpaka ikakaribia
masikio yake, kisha akauweka wa kulia juu ya upande wa nyuma wa mkono wa
kushoto."
Ibni Khuzaymah katika sahih yake na Annasai na Abu
Daud katika Sunan yake na Ahmad katika Musnad yake 4/318 na Ibni Majah katika
Sunan yake 1/266 na Addarimiy katika Sunan yake 1/314 na Ibnil Jarood katika Al
Muntaqa hadithi nambari 208 na katika vitabu vingi vingine".
Nadhani dalili hizi zinatosha kutujulisha kuwa kukunja mikono ni Sunnah
iliyothibiti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (SAW), lakini pia ninapaswa
kuhakikisha kuwa nimepitia vitabu vingi vya Fiqhi na sijaona hata mahali
pamoja palipoandikwa kuwa kutokunja mikono kunabatilisha sala.
Kukunja mikono si katika Masharti ya Sala wala si katika Nguzo zake wala si
katika Fardhi zake, bali hiyo ni katika Sunnah zake, mwenye kukunja anapata
thawabu na asiyekunja hapati dhambi, na Sala yake ni sahihi mia fil mia.
Wallahu taala aalam
Wassalaam alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh
Ndugu yenu
Muhammad Faraj Salem