KUHITILAFIANA
Inajulikana wazi kabisa na kila mtu kuwa;
Watu wanahitilafiana katika fikra zao. Mwanadamu tokea alipoumbwa alikuwa
akiutizama ulimwengu kwa mtazamo wake, kila mmoja kwa mtazamo wake na kwa
falsafa yake. Na kwa ajili hiyo wakakhitilafiana katika mtazamo wao, katika
kupenda kwao na katika kuchukia kwao. Na kila ulimwengu unapopiga hatua katika
maendeleo, katika majenzi, katika kupanuka kwa miji, hitilafu za wanadamu
zinaongezeka na kupanuka. Na kwa ajili hiyo zikatokea hitilafu mbali mbali za
ki Madhehebu ya kifalsafa, hitilafu za kijamii na za kiuchumi.
Mmoja katika wana falsafa wa zamani
anasema;
“Haki yote, haiwezekani ikamilikiwa na
upande mmoja , wala kukosewa yote na upande mwingine, bali kila upande husibu
sehemu yake. Mfano wake ni mfano wa kundi la watu vipofu waliotakiwa kwa muda
mfupi sana wamwendee tembo na kumgusa, kisha wamuelezee jinsi alivyo.
Yule aliyeshika mkongwe, akasema;
“Mwili wa tembo uko duara mfano wa gogo
la mti”,
Aliyeushika mgongo akasema;
“Mwili wa tembo upo mfano wa jabali
dogo”,
Aliyeshika sikio akasema;
“Mwili wa tembo mpana pana duara na
laini”.
Na hivyo hivyo kila mmoja atauelezea
mwili wa Tembo kiasi alivyodiriki kuugusa. Kila mmoja kati yao anasema kweli,
lakini anaelezea kinyume na mwenzake na kudhani kuwa anavyojuwa yeye ni sahihi
na kwamba wenzake wamekosea.
Tizama jinsi gani ukweli
ulivyowaunganisha na tizama jinsi gani kukadhibishana kulivyowatenganisha.
Kila mmoja alivyoisibu sehemu tu ya haki
na kudhani kuwa yeye ndiye mwenye kuijua yote.”
Hitilafu husababishwa na mambo mengi,
yakiwemo kupenda, matamanio ya nafsi, mielekeo ya elimu, ya kifikra, kuiga
waliotangulia, kupenda umaarufu, kupenda ukubwa, hitilafu za ustaarabu na ziko
sababu nyingi nyingine na maelezo yake ni mengi sana tutayazungumzia siku za
usoni Inshaallah itapohitajika.
MUHAMMAD
FARAJ SALEM AL SAIY