EDA
Muhammad
Baawazir
Eda ni kipindi anachokaa mwanamke
aliyeachika au aliyefiwa na mumewe, na baada ya kipindi hicho ndoa yake huwa
halali. Na imeitwa eda kwa jina hili kutokana na jina la kiarabu ‘iddah’ kwa kukusanya kwake (idadi) ya
miezi au ‘quruu’*1 au hedhi au vipindi vya tohara ya hedhi.
HEKIMA YA KUHALALISHWA EDA
Hapa tunaona baadhi ya mawazo ya wanachuoni ambao wameona hizi
ndizo hekima au sababu za kuwekewa eda sheria, ingawa hekima ya mwanzo na ya mwisho ni hiyo ya mwisho hapo chini ya fungu hili:
- Kutambua kama
mwanamke ni mjamzito au la.
- Kuweza kubainika nasaba au kizazi ili kuepusha utata wa kutokujulikana nani ndiye baba.
- Kipindi ambacho mke anakaa eda kiwe kifupi au
kirefu kinaangaza mwangaza wa kweli kuhusu uzito
wa ndoa yao na mkataba mtakatifu walioufunga baina yao.
- Eda ya kufiwa inamwezesha mwanamke kutoa
huzuni zake na kupata muda wa kujiliwaza na msiba
uliomtokea wa kipenzi chake. Pia inamhifadhi kwa
kutokuwa chombo cha kusemwa na kuzungumzwa kila apitapo.
- Kupata nafasi mume na mke kutafakari kwa makini
kuhusu mahusiano yao
kabla hawajavunja muungano wao wa kifamilia na haswa katika talaqa
ivunjikayo (ya kwanza au ya pili)
- Ama HEKIMA ya juu kuliko zote kuhusu edda ni UTIIFU kwa maamrisho ya Mola wetu Subhaanahu
Wataala. Kwani kuna wengi wanaotoa hoja za akilini mwao kama vile kudai
kuwa siku hizi kuna utaalam wa kujua kama mwanamke ana mimba kwa vipimo
bila haja ya kukaa eda mwanamke n.k. Hoja kama hiyo si ya busara maana ni
sawa na kusema ‘siku hizi kuna kinga za mimba kama kondomu n.k, kwa hiyo zinaa
iwe halali!’ Wamesahau kuwa HEKIMA kuu ni UTIIFU
kwa Muumba na Utekelezaji wa MAAMRISHO yake na mengine ni ya ziada na wala
si ya msingi. Mwenyeezi Mungu anatujua zaidi kuliko tujijuavyo nafsi zetu.
HUKUMU ZA EDA
1- Eda kisheria: Kisheria eda ina
maana nyingi, mojawapo: Kupata yakini kwa kile kiumbe chenye kuzaliwa ili
kuepukana na mchanganyiko wa nasaba. Na vilevile eda hekima yake hiyo eda ni kutoa fursa na muda kwa mume na mke baada ya talaka
huenda kwa kipindi hicho wakamaliza tofauti zao na kurudiana na kuishi tena kama wanandoa kamili. Na pia sababu
nyingine ni kulipa na kutekeleza haki haki zote za
mume aliyefariki (ikiwa ni eda ya kufiwa) na kudhihirisha athari za kumpoteza
mume, kwa kipindi cha maombolezi, nako ni kujizuia huyo mwenye eda na kujipamba,
kujiremba n.k kama tutakavyoona mbele.
Na eda ni wajibu kwa
mwanamke wakati anapoachana na mumewe, ima kwa talaka au kwa kufiwa na mumewe
au ‘faskh’ (kutenguka kwa ndoa) au ‘khul’u’*2 (kujivua na ndoa hiyo). Na
ni sharti awe ashaingiliwa na mumewe. Na eda haiwi kwa
mwanamme, na anaruhusiwa kuoa mwanamke mwingine bila hata kusubiri kwisha hiyo eda ya
mkewe. Ila tu kama kutakuwa na kizuizi, kama kutaka kumuoa dada ya mkewe, maana
hairuhusiwi kisheria kuchanganya baina ya dada wawili kwa wakati mmoja kwani kisheria
atakuwa yule mke aliyempa talaka ni wake hadi atakapomaliza muda wa eda yake.
Au pia kama ana wake wanne na amempa talaka mmoja kati yao, haitoruhusiwa kwake kuoa mwanamke
mwingine hadi eda ya huyo aliyemuacha imalizike vilevile. Kisheria hairuhusiwi
kuwa na zaidi ya wake wanne.
2- Kumalizika eda: Kunatofautiana muda wa
kwisha eda kutokana na sababu au aina za eda yenyewe. Aina zenyewe ni hizi zifuatazo:
a) Eda ya aliyepewa talaka: Ni ‘quruu’*1 (vipindi
vya hedhi/tohara) tatu, endapo atakuwa keshaingiliwa na
mumewe na hakuwa ni mwenye mimba, au aliyekoma hedhi, au mdogo asiyepata hedhi
bado. Na haya yamefafanuliwa na Mwenyeezi Mungu S.W.T
aliposema: {{Na wanawake walioachwa wasubiri (wasiolewe) mpaka tahara
tatu ziishe…}} AL BAQARAH 228
b) Eda ya aliyefiwa na mumewe: Ni miezi minne na siku kumi,
kama alivyoipangia Mwenyeezi Mungu katika
qur’an: {{ Na wale wanaofishwa
(wanaokufa) miongoni mwenu na kuacha wake; hawa (wake) wasubiri (wasiolewe)
miezi minne na siku kumi.}} AL BAQARAH 234. Kiwango hiki ni endapo atakuwa si mjamzito (mwenye mimba), ama akiwa ni
mjamzito basi eda yake itakwisha pale atakapojifungua. Kama tutakavyoeleza zaidi
hapo mbele.
Hakuna tofauti ya huyu aliyefiwa ikiwa mumewe alimwingilia
alipokuwa hai au hakumwingilia, yote ni mamoja. Na
atakapokufa mume na hali mkewe yuko katika eda ya
talaqa rejea, itageuka eda hiyo na kuwa ni eda ya kufiwa. Ila endapo mume wa
mke aliyeachwa talaka wazi atakuwa amekufa, na kumuacha kwake kulikuwa wakati akiwa
na afya yake nzuri au kwa matakwa ya mwanamke mwenyewe, basi katika hali hiyo
mke atakamilisha tu hiyo eda ya talaka na hatokaa eda ya kufiwa.
c) Eda ya aliyekoma hedhi: (Kwa kupindukia miaka) Ni miezi
mitatu kama alivyosema Mwenyeezi Mungu: {{ Na wale waliokoma kutoka hedhi miongoni mwa wake
zenu, ikiwa mnayo shaka (katika muda wao wa eda), basi muda wao wa eda ni miezi
mitatu…}} AT TWALAAQ 4. Na itakapowarejelea hedhi
wakati ashaanza eda yake, basi atakaa eda ya ‘quruu’*1 badala ya miezi.
Ama akiwa amepata hedhi mara moja au mbili tu kisha akawa
katika hedhi yake iliyokoma basi arejee kwenye kukaa eda ya miezi mitatu badala
ya ‘quruu’.
d) Eda ya mjamzito (mwenye mimba): Inamalizika kwa
kujifungua kama anavyosema hapa Mwenyeezi Mungu S.W.T. : {{ …na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa.}} AT TWALAAQ 4
Ama ikiwa mwanamke eda yake ishaanza naye hajui kama ana mimba na baadaye ikadhihiri hiyo
mimba, basi atabadili eda yake kutoka kuwa ni eda ya ya mwezi na kuwa ni eda ya
mimba (ujauzito). Na ataendelea na eda hadi atakapojifungua.
e) Eda ya msichana ambaye hajafikia kupata hedhi, na eda ya
mwanamke aliyevunja ungo ambaye pia hajawahi kupata hedhi na ambaye hakufikia
umri wa kukoma hedhi: Hawa wote eda yao ni miezi mitatu kutokana na
ushahidi wa maneno yake Allah: {{ Na wale
waliokoma kutoka hedhi miongoni mwa wanawake wenu, ikiwa mnayo shaka (katika
muda wao wa eda), basi muda wa eda yao ni miezi mitatu, na (ndio muda wa eda
kwa wale) ambao hawajapata hedhi bado.}} AT TWALAAQ 4.
Lakini endapo itamtokezea hedhi mmoja kati ya wanawake wa aina hiyo kabla ya
kumalizika muda wa
eda yake, ataibadili hiyo eda na kuwa ni
ya ‘quruu’*1 badala ya ile ya miezi iliyokuwa mwanzo.
f) Eda ya mwanamke aliyezaa mapacha au zaidi: Itaanza baada
ya kumzaa pacha wa mwisho, kwani mazingatio katika eda
ya ujauzito ni kujulikana kiumbe (bara-atu rahim), yaani kuondokana kabisa na
ujauzito.
g) Eda ya aliyetowekewa na mumewe:
Aliyetoweka ni yule ambaye hajulikani alipo na habari zake hazikusikika tangu
alipoondoka au kutoweka pamoja na kutafutwa kwa muda mrefu. Wanachuoni wa sheria wametenganisha kati ya kupotea kwake kwa aina
mbili: kujulikana alipo na kutojulikana. Ikiwa alipo panajulikana na ikiwa yuko
salama huko alipo ima kibiashara, kikazi au kimatembezi, na kukatika habari
zake, basi wamesema wanachuoni kuwa ndoa yao bado itabaki hadi kuthibitike mauti
yake au atoe talaqa au kupite muda mrefu ambao si wa kawaida ya yeye kupotea
hivyo. Ikifikia hali hiyo, basi mke atakaa eda na
kisha itakuwa halali kwake kuolewa tena. Ama ikiwa kupotea kwake kut ajulikana kama vile kumesikika kuwa ndege aliyopanda
katika safari yake imeanguka na hakupona mtu au gari alilosafiria limepinduka
n.k, hapo mke atakaa eda ya mfiwa ya miezi minne na siku kumi. Na ikiwa kupotea
kwake kumekuwa kurefu mno na hajulikani kama kapatwa na nini, na kukawa hakuna
mawasiliano ya aina yoyote, basi hapo mke atasubiri kipindi cha miaka minne
kisha atakaa eda ya mfiwa ya miezi minne na siku kumi. Ila
ni vizuri zaidi kabla ya hivyo kuwe kumefanyika majuhudi makubwa ya kumtafuta
kwa kutumia njia za kila aina na haswa kwa wakati huu ambapo njia za
mawasiliano zimekuwa nyingi na nyepesi mno. Ni vizuri kutolewe taarifa kwenye
vyombo vya habari, mitandao, mabalozi n.k Lakini ikiwa kutoweka kwa bwana
kukawa hatimaye kumebainika alipo na kukawa na mawasiliano, m athalan
kumejulikana kuwa yuko jela na kifungo chake ni miaka mingi, au kasafiri mbali
na atakawia sana kurudi, hapo kutatazamwa kama muda huo mrefu utamuathiri mke
na watoto wake ima kiuchumi au kimwili au kiusalama, basi hapo mke ana haki ya
kusubiri au kudai talaqa au kuomba kuachishwa na mume huyo. Qadhi au Imam au
kiongozi wa dini ataangalia sababu za pande zote na
dharura iliyopo kabla ya kumwachanisha mke na mumewe.
3- Yanayopaswa kwa mwenye eda:
Wanachuoni wengi wa kisheria wamekubaliana kuwa mwenye eda anapaswa kukaa
katika nyumba ya ndoa kwa muda wa eda yake yote hadi itakapomalizika. Ikiwa eda
hiyo ni ya talaqa au ya kuomba kuachwa (kuachishwa) au
ya kifo, haitakikani atoke ila kwa haja maalum au nyudhuru za kisheria la sivyo
atakuwa ametenda dhambi. Na mume anaweza kumkataza asitoke ikiwa eda hiyo ni ya talaka, na mrithi ana haki ya kumzuia kutoka ikiwa eda
hiyo ni ya kufiwa. Ila baadhi ya wanachuoni wanasema
kuwa katika eda ya kufiwa mke anakaa eda yake atakavyo.
Na inapaswa kwa mwenye eda ya kufiwa akae
katika maombolezi (al ihdaad) kwa muda wote wa eda yake. Na kuomboleza ni kuacha yeye kujipamba kwa mavazi ya marembo rembo, kuvaa
dhahabu, na kujipaka manukato n.k. Kufanya hivyo kuna maana ya kuchunga na
kuheshimu ule uhusiano wa kindoa uliokuwa baina yake na mumewe, nako pia ni
kuonyesha utiifu kwa uhusiano wao. Pia kunapatikana katika huo muda wa maombelezi, utulivu wa nafsi ya mwanamke na kufikiria
maisha mapya ya ndoa yamkabiliyo mbeleni.
MAMBO MBALIMBALI KATIKA EDA NA HASWA
EDA YA KUFIWA
Haya ni baadhi
ya mambo ambayo ni haramu kwa mwenye eda kuyafanya kisheria:
- Kujitia manukato
mwilini au nguoni.
- Kujitia rangi za
mdomo, rangi za kucha, poda, na aina zote za
vipodozi.
- Kujitia wanja wa macho bila dharura ya kuumwa.
- Kuvaa nguo za rangi
rangi: au ya rangi moja lakini yenye kuvutia na
yenye mapambo. Si lazima hata hivyo kuvaa kaniki kama inavyodhaniwa na wengi au shuka la bafta n.k.
- Kuvaa mapambo ya
dhahabu, fedha, lulu, almasi na madini mengine,
ikiwa ni pete, mkufu, hereni, bangili na vinginevyo.
- Kujitia hina popote
maungoni panapoonekana na watu.
- Kutoka nje pasipo na dharura. Haikatazwi mwenye eda kutoka nje kama hana wa kumtegemea kwa mahitaji yake,
mathalan ikiwa inambidi kufanya kazi kwa kupata mahitaji yake, kwenda
kununua mahitaji yake ya nyumbani, au kufundisha kama mwalim n.k.
- Kuolewa
- Kuposwa
MAMBO YA UZUSHI YANAYOFANYWA NA WAKAA
EDA
Kuna mambo yafanywayo na baadhi ya wanawake wenye kukaa eda ambayo ni ya kijahili
na hayapo katika mafunzo ya dini yetu hii nyepesi. Mambo hayo ima kwa kutokujua hao wayafanyao, au kwa kufundishwa na
maustaadh na masheikh wababaishaji.
Utakuta baadhi ya wenye eda hawawezi
kutoka majumbani mwao sharti wawe wametoka na fimbo au
bakora, wengine wakitoka huku wamevaa matambara kama mwendawazimu, na wengine ambao
hawajistiri inavyopasa utawaona nywele zao hawazichani wala kuzisafisha kwani
wameambiwa hairuhusiwi kuchana wala kuoga kila mara. Hadi mwanamke akimaliza
eda yake, si chawa na uvundo unaotoka mwilini mwake
kwa kutojisafisha kila mara. Hayo ni matunda ya
mafunzo ya waalimu wa dini wasio na elimu sahihi ya kutegemewa.
Haya ni baadhi
ya mambo ya uzushi katika eda yaliyokuwa yakifanyika zamani na yanayofanyika
hadi sasa katika jamii yetu:
- Kuja mtu kama mwalimu au sheikh kumnuiza huyo mwenye eda
wakati aanzapo eda yake, na kumchagulia saa ya kuianza hiyo eda.
Eda huanza pale tu
akatapo roho mume. Hakutakikani kunuizwa wala
kungojea saa maalum ya kuianza.
- Baadhi ya wenye eda
huwa na khofu na eda na kuamini kuwa ikiwa
hajakaa hiyo eda ipasavyo, basi atafikwa na balaa au wazimu au kifo.
- Kutonyanyua sauti ili isisikike na watu walio nje. Si vizuri mwanamke
kunyanyua sauti yake lakini kwenye hili kunakuwa kunatiliwa mkazo mno hata
inakuwa vigumu watu kumsikia, hata kama anahitaji kitu au anamuhitaji mtu amjie,
matokeo yake anakuwa kama bubu au yuko kifungoni hata baadhi ya
mahitajio yake anayakosa kwa kuamini kuwa hapaswi kutoa sauti.
- Kupelekwa chooni kwa kuchukuliwa vyetezo vya ubani, na yeye kubeba fimbo
ya mumewe au kisu au kukamata kaa la moto lililozimika, au ndimu, au
chumvi.
- Wengine hawaendi
chooni usiku kwa kuamini ni vibaya na huwa
wanawekewa chombo chumbani cha kujisaidia haja zake. Matokeo chumba
kinakuwa hakitamaniki na kuhatarisha pia afya ya
mkazi.
- Hata akiwa faragha
hawezi kutoa kitambaa cha kichwa akiamini kuwa ni
balaa. Kwa maana amefundishwa kuwa akifanya hivyo atatoa nafasi ya wazimu
kumuingia kichwani mwake.
- Kutoruhusiwa
kulalia kitanda chenye godoro na badala yake
alalie kitanda cha kamba au mbao kisicho na tandiko juu yake au jamvini.
- Kuvaa aina fulani ya viatu tu, kama vya mbao na sharti visimtoke mguuni. Na
wanaamini kuwa kiatu kikimvuka tu basi na wazimu
umemvaa saa hiyo hiyo.
- Kukatazwa kuonana na wanaume hata kama ni maharimu wake.
- Kutoruhusiwa kusema na
mtu tokea alasiri ya siku ya alkhamis tena baada ya kuogeshwa! Hadi mshuko
wa siku ifuatayo ya ijumaa. Hata akitokewa na hatari hawezi kupiga yowe la kuhitaji msaada!
- Kulazimishwa
kufunga saumu siku hizo za alkhamis na ijumaa na kusoma
qur’an na nyiradi ndefu ndefu. Haijulikani kama
saumu hiyo ni ya eda au ya nini, na wala haijulikani ilipofundishwa.
- Kuja kusomewa kila
alkhamis na huyo mwenye kumsomea hupewa chochote.
Naam, hayo ndiyo hao masheikh wababishaji wayafundishayo ili waweze kupata chochote. Na mambo mengi ya dini
yamezushwa ili kuwanufaisha hao wayaanzishayo.
M.Mungu awaongoze.
- Kukatazwa hata
kujitazama katika kioo kwa muda wa eda yake yote.
- Kutoamkia au
kutoamkiwa kwa kupewa salaam kama kuambiwa ‘anakusalimu fulani’ bali huambiwa
‘Fulani anakupeni hujambo?’
- Kutojibu neno
lolote katika hali ya kusimama. Ila ni sharti
akitaka kumjibu mtu, apige magoti ndipo ajibu.
- Kulalia kitu
kinachomhusu marehemu chini ya mto. Au kulalia ndimu, msumari na wembe.
- Kutokukata kucha za
mikono wala za miguu kwa muda wote huo wa eda wa
miezi minne na siku kumi. Nako ni kufuga uchafu
na kujihatarisha yeye mwenyewe kujidhuru kwa makucha yake.
- Kuzikusanya nywele
zote zilizong’ooka ili ziende zikatupwe mbali
kabisa kama baharini siku atokapo eda yake pamoja nywele
anyolewazo siku hiyo.
- Kuondoshwa hiyo eda
katika sehemu za pwani, kwa kuchagua siku maalum
na kwenda kuosha nguo pwani na kugonga madebe na vyuma na kukaa siku tatu
bila kuonekana na watu.
Haya ni mambo
yaliyokuwa yakifanywa zamani na mengine hadi leo yanaendelea kufanyika katika
baadhi ya jamii yetu kutokana na kudanganywa watu na pia kwa kutokuelewa wengi
wetu na kwa kutofanya jitihada za kujielimisha. Alhamdulillah hivi sasa
kutokana na kwamba elimu sahihi imeenea sehemu nyingi
na wengi wanasoma, basi mambo hayo yamepungua sana.
Mambo yote yaliyopo hapo juu, mengi ni ya kusikitisha na mengine ni ya kuihusisha dini yetu na
ugumu na kuipa picha mbaya kabisa.
Mwenyeezi Mungu anasema: {{ …wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini}}
AL HAJJ 78.
Pia anasema vilevile: {{…Mwenyeezi
Mungu anakutakieni mepesi wala hawatakieni magumu}}AL
BAQARAH 185
Vilevile tumeona mifano mingi ambayo
Mtume s.a.w. alikuwa akisisitiza kuhusu kutotia uzito na
ugumu katika dini. Alikuwa akisema: ‘‘Nimeletwa kufundisha dini ya Uislam
iliyo nyepesi’’ Pia alipowatuma Ali r.a. na
Muadh bin Jabal r.a kwenda Yemen, aliwausia kufanya wepesi kwa
kuwabashiria kheri watu wa huko na kuwavuta katika dini kwa upole bila
kuwatilia uzito na kuwakimbiza.
Sasa ni ajabu
kuona baadhi ya masheikh wakiwafundisha watu mambo magumu magumu na yasiyokuwa
hata katika mafundisho ya dini yetu hii nyepesi.
Mwenyeezi Mungu atujaalie hima ya
kujifunza na kutafuta elimu ya haki na iliyo sahihi,
na atuepushe na uzushi na ya batili.
-----------------------------------------------------------------------------------------
*1 QURUU: Kuna kutofautiana kwa maoni ya
wanachuoni kuhusu hii ‘quruu’, je, ni tahara au ni hedhi?
TOFAUTI YA
MAULAMAA JUU YA QURÛU
Qurûu, ni neno linalotumika kwa maana ya hedhi au tahara kwa vile
linaoana na maana zote mbili. Hanafi na Hanbali,
wanaona kwamba neno hili lina maana ya hedhi. Hii inamaanisha
kwamba mwanamke aliyeachwa atakaa hadi hedhi tatu zimalizike. Ikiwa
hedhi itakatika baada ya mara moja tu, basi itakamilishwa na
miezi.
Ama Maalik na Shaafii, wao wanaona kwamba neno hili lina maana ya
tahara. Na tahara hapa ni vile vipindi vinavyokuwa
baina ya hedhi mbili.
*2 KHULUU:
Kilugha: Ni neno lenye asili ya Kiarabu lenye
kumaanisha kuondosha na kuvua. Ni kama
vile mtu anavyoivua nguo kuitoa mwilini.
Kisheria: Ni kukiondosha kifungo cha ndoa kwa tamko la kuvua au kwa tamko lingine lenye maana kama hiyo kwa mkabala wa mali anayoitoa mke kumlipa mumewe. Na hi li
bila shaka limeruhusiwa ili kumpa mwanamke uhuru wa
kujiengua toka kwenye ndoa na mumewe baada ya maisha kwa upande wake kufikia
ukomo wa kutoweza tena kuishi kwa raha na mumewe.
Dalili yake: Ni aya ya 229 ya Surat Al Baqarah,
Mwenyeezi Mungu anasema:{{Talaka (unazoweza
kumrejea mwanamke) ni (zile zilizotolewa) mara mbili (za kwanza). Kisha ni kumweka kwa wema au kumwacha kwa ihsani (Wala usiweze
kumrejea tena mpaka aolewe na mume mwengine maadam ametimiza mara tatu katika
kumwacha ukimrejea). Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlichowapa (wake
zenu), isipokuwa (wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka
ya Mwenyeezi Mungu, hapo itakuwa hapana dhambi kwao (mwanamme wala mwanamke
katika) kupokea (au kutoa) ajikomboleacho < /SPAN>mwanamke. Hii ndio mipaka ya Mwenyeezi Mungu; basi msiiruke. Na
watakaoivuka mipaka ya Mwenyeezi Mungu, hao ndio madhalimu (wa nafsi zao) }}.
Ama kwenye Hadithi ni kile kisa cha mke
wa Thaabit bin Qays aliyekwenda kushtaki kwa Mtume juu ya mumewe, pamoja na
kuwa mumewe hakuwa na tatizo la dini wala tabia bali yeye hakumpenda na akawa
anakhofia kutotekeleza wajibu wake kama mke. Mtume aliwatenganisha lakini kwa
kumtaka mke airejeshe bustani aliyokuwa amepewa na mumewe kama ni mahari. Hadithi
hiyo ipo katika sahihi al Bukhari 5273.