ITIKADI ZISIZO SAHIHI

 

Funga YaAshuraa
Baina Ya Wenye Kupinga
Na Wenye Kuunga
Mkono

 

Muhammad Faraj Salem Al Saiy

 

Tukio la ‘Ashuraa ni tukio muhimu sana kwa walimwengu wote kutoka wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu Muusa (‘Alayhi swalaatu was-salaam) hadi wakati wa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ndani ya siku hii aliuliwa kwa dhulma Al-Hussayn (Radhiya AllaahuAnhu) kipenzi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam) na bwana wa vijana wa peponi. Aliyekuwa mfano mwema wa kuigwa na Ummah wote kutokana na hikmah yake na wema wake aliourithi kutoka kwa babu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam), na sisi tunajitenga mbali kabisa na kila aliyeshiriki katika mauaji hayo mpaka siku ya Qiyaamah.

 

Masuala sasa yanakuja:

 

Yafuatayo ni majibu ya masuala yaliyotangulia:

1 - Kutoka kwa Abul-Hassan (‘Alayhi swalaatu was-salaam) kuwa amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam) ameifunga siku yaAshuraa."

 

[Tahdhiybul-Ahkaam 29/4, Al-Istibsaar 134/2, Al-Wafi 13/7, Wasailush-Shia 337/7, Jami’ah Ahaadiythush-Shia 475/9, Al-Hadaaiqun-Naadhirah 370-371/13, Funga yaAshuraa ukurasa 112].

 

2 - Kutoka kwa Abu Ja’afar (‘Alayhi swalaatu was-salaam) kuwa amesema: "Funga ya Ashura inafuta madhambi ya mwaka mzima."

 

[Tahdhiybul-Ahkaam 300/4, Al-Istibsaar 134/2, Jami’ah Ahaadiythush-Shia 475/9, Al-Hadaaiqun-Naadhirah 371/13, Swiyaamul-‘Ashuraa ukurasa 112, Al-Wafi 13/7, Wasailush-Shia 337/7].

 

3 - Kutoka kwa As-Swaadiq (Rahimahu Allaahu) kuwa amesema: "Mwenye kufunga Muharram anajikinga na kila ovu."

 

[Wasailush-Shia 347/7, Al-Hadaaiqun-Naadhirah 377/13, Jami’ah Ahaadiythush-Shia 474/9].

 

4 - Na Kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: ((Swalah bora baada ya zilizofaridhishwa ni ya usiku wa manane, na funga bora baada ya mwezi wa Ramadhaan ni Funga ya mwezi wanaouita Muharram.)) [Masdari zilizotangulia kutajwa]

 

Baada ya kuzisoma kauli hizi za maulamaa mbali mbali wenye kusifika wa Madhehebu ya Kishia walizoziandika ndani ya vitabu mbali mbali vinavyoheshimika, inatuwia wazi kuwa haijuzu kuikanusha swaumu hii yaAshuraa na kudai kuwa eti imeanzishwa na watawala wa kabila la Bani Umayyah.

 

Funga hii ni Sunnah yenye uhakika iliyothibiti ndani ya vitabu vya madhehebu mbali mbali ya Kiislamu, na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni mfano mwema wetu sisi wa kumfuata, ameifunga siku hii na akatutaka na sisi pia tuifunge.

 

Anaweza mtu kwa kuuendekeza moyo wake na kwa kufuata matamanio ya nafsi yake akasema kuwa: “Hizi ni hadithi za uongo zilizozushwa tu.” n.k, lakini mwenye kuutafuta ukweli mara baada ya kuiona haki hatoweza kusema maneno haya, bali atasalimu amri na kuifuata Sunnah hii tukufu. Kwani moyo wa aliyeamini kikweli haukubali kufuata matamanio ya nafsi. Haukubali kufuata isipokuwa haki tu itokayo kwa Mola wake kupitia kwa Mtume wake mtukufu (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ewe ndugu yangu Muislamu! kumbuka kuwa hapana baada ya haki isipokuwa upotovu, na uikumbuke kauli ya ImaamAliy (Radhiya AllaahuAnhu) aliposema:

"IfungeniAshuraa siku ya tisa na ya kumi akiba ya maneno kwani inafuta madhambi ya mwaka uliotangulia.” [Mustadrakul-Wasaail 1/594 na Jami’ah Ahaadiythush-Shia 475/9].

 

Na kutoka kwa IbniAbbaas (Radhiya AllaahuAnhu) kuwa amesema: "Utakapouona mwezi wa Muharram anza kuhesabu, na itakapotimia ya tisa basi funga kuanzia asubuhi ya siku hiyo." Anasema mwenye kuisimulia Hadiyth hii kuwa aliuliza: "Mtume wa Mwenyezi Mungu alifunga hivi pia?" Akasema IbniAbbaas (Radhiya AllaahuAnhu): "Ndiyo." [Iqbaalul-A’amaal ukurasa 554, Wasailush-Shia 347/7, Mustadrakul-Wasaail 594/1].

 

Kumbuka pia ndugu yangu kuwa riwaya zote zilizokuja zenye kuitilia nguvu swaumu hii zimekuja kwa njia sahihi na zile zote zenye kuipinga swaumu hii zimekuja kwa njia dhaifu kama alivyokiri Ash-Shaykh Al-Hajj As-Sayyid Muhammad Ridha Al-Hussayn Al-Hairi katika kitabu chake kiitwacho Najatlul-Ummah Fiy Iqaamatul-Azaa Li A’al Hussayn Wal-Aimmah ukurasa wa 145, 146 mpaka 148.

 

Je ndugu yangu baada ya ushahidi huu utatanguliza maneno ya watu wa kawaida au utatanguliza maneno ya mbora wa viumbe vyote (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam)?

 

Tanbiyh:

 

Mauaji ya Al-Hussayn (Radhiya AllaahuAnhu) ni mojawapo ya masaibu makubwa waliyokumbwa nayo Waislamu, na kubwa zaidi ni kuuliwa kwa baba yake ImaamAliy bin Abu Twaalib (Radhiya AllaahuAnhu) na kubwa kupita yote ni kufariki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahualayhi wa aalihi wa sallam). Muislamu anapokumbwa na masaibu anatakiwa akumbuke masaibu haya matatu ili aweze kuona na kuhisi kuwa masaibu aliyokuwa ndani yake ni madogo sana akiyalinganisha na hayo.

 

Hata hivyo Mwenyezi Mungu Ametufundisha katika kitabu chake kitukufu kuwa Muislamu anapokumbwa na masaibu aseme: "Innaa liLlaahi wa innaa ilayhi raaji’uun."

 

Mwenyezi Mungu Anasema: {{Ambao uwapatapo msiba husema: "Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Yeye sisi tutarejea.” Hao juu yao zitakuwa barakah zitokazo kwa Mola wao na rehema, na ndio wenye kuongoka.}} [Al-Baqarah: 156-157]

 

Na kumbuka kuwa Al-Hussayn (Radhiya AllaahuAnhu) ni shahiyd aliyeko peponi akineemeshwa na Mola wake, na kwamba ishapita miaka elfu nyingi tokea alipouliwa kwa dhulma, na wajibu wa Muislamu ni kusubiri na kuomba na sio kutukana na kukufurisha.

 

Anasema At-Tijani ambaye ni mwandishi maarufu wa kitabu 'Then I was guided' (Thumma Ihtadayat) kuwa: "Mengi kati ya wanayofanya watu hivi sasa katika kuomboleza kifo cha Al-Hussayn (Radhiya AllaahuAnhu) hayakupata kufanywa na yeyote tokea alipokufa Mtume wa Mwenyezi Mungu hadi siku hii ya leo na wala hayakuwahi kufanywa na Al-Hassan wala Al-Hussayn (Radhiya AllaahuAnhu).”

 

Anasema kuwa mmoja katika aliyeshuhudia mauaji hayo yaliyofanyika Karbala amesema: "Nimehudhuria mkusanyiko usiopata kuhudhuriwa na mtu yeyote, na nikashuhudia kwa jicho langu yale ambayo hakupata kuyashuhudia mtu yeyote hapo Karbala alipouliwa baba yangu na ami zangu na ndugu zangu wote, na nikaona masaibu yanayoweza kuyaondoa majabali."

 

Anasema At-Tijani: "Juu ya yote hayo aliyoyaona lakini hajapata kufanya haya yanayofanywa siku hizi wala kuamrisha watu wake kufanya hivyo." [Kitabu cha 'Kullu-l-huluul' ukurasa wa 151].

 

Anaongeza At-Tijani: "Hata ajitahidi vipi mwenye kujitahidi, lakini lazima aelewe kuwa hayo wanayotenda katika kupiga vifua na kuomboleza na kulaani na kutukana sio katika maamrisho ya diyn hata kama watatoa fatwa wenye kutowa, lazima waelewe kuwa hayo ni katika hisia zinazopindukia mipaka." [Kitabu cha 'Kullu-l-huluul' ukurasa wa 148].